November 24, 2024

Namna huduma kwa wateja inavyoweza kukuza brand ya biashara

Lugha nzuri ni asali ya kuvutia wateja wengi, jeuri na dharau vitatakurudisha nyuma na jitahidi kujenga mwenekano unaowavuta wateja wengi kwa kuwa msafi na kuweka mazingira ya biashara vizuri.

Wateja wenye furaha huchochea kukua kwa brand yako kwa kiwango kikubwa. Jitahidi kutoa huduma bora kwa wateja. Picha|Lyfe Marketing.

  • Jitahidi kujenga mtazamo chanya kwa wateja juu ya biashara au huduma zako
  • Lugha nzuri ni asali ya kuvutia wateja wengi, jeuri na dharau vitatakurudisha nyuma.
  • Jitahidi kujenga mwenekano unaowavuta wateja wengi kwa kuwa msafi na kuweka mazingira ya biashara vizuri.

Wengi huenda hutumia nguvu nyingi kutafuta maana rafiki ya ‘brand’ au nembo. Huenda hushindwa kupanga mikakati makini kujipanua kisoko kwa kukosa tu maana ya neno hilo.

Kikubwa, unachopaswa kufahamu ni kwamba brand ni mtazamo, hisia, historia waliyonayo watu juu ya bidhaa au huduma husika.

Hii huusisha namna ambavyo watu wanaizungumzia bidhaa yako au huduma na namna bidhaa au huduma huonekana kwa macho ya mtumiaji wa mwisho. Lakini kama haitoshi, brand huusisha hisia anazopata mtumiaji wa bidhaa au huduma yako.

Yote hayo yanatokea iwapo tu kuna kitu ambacho huitwa huduma kwa wateja. Huduma kwa wateja ni moyo wa biashara yeyote duniani.

Watu wengi walio katika biashara wamekuwa wakidhani kuwa bidhaa bora au huduma nzuri ndiyo njia pekee ya kufanya biashara zao kukua na kupanuka Zaidi.

Hii si kweli kwa kuwa “ukishindwa kuwasiliana vizuri na mteja wako umeshindwa kufanya biashara”.

Ili kufanikiwa katika biashara, kuna vitu vingi vya kuzingatia katika kukuza na kuifanya idara ya huduma kwa wateja iweze kukidhi matarajio ya mteja au mdau yeyote kwenye biashara husika.


Jenga mtazamo chanya

Kabla ya kuweka mikakati yeyote ya kuboresha huduma kwa wateja, wapaswa kujihoji maswali kadha wa kadha kwa mfano; mteja kwako ni nani, unamchukuliaje, unampa nini zaidi ya huduma uliyonayo, mteja unamwambia nini asiporidhika na huduma yako, mteja anakuwaje balozi wa biashara yako na mteja ni wa aina gani.

Ni vyema ukayapatia majawabu maswali hayo ili yakusaidie kupata mwelekeo wa namna ya kukuza kanzidata (database) ya wateja na wadau wakubwa ili wawe mabalozi wa biashara yako huko nje.

Kumbuka njia kubwa na yenye maana katika kukuza masoko ni njia ya mdomo (Word of mouth marketing strategy.)


Kuwa na lugha nzuri

Katika eneo hili kwenye biashara kuna lugha za aina mbili yaani lugha ya sauti (verbal language) na lugha ya alama na mwili (body and sign language).

Lugha hizi zina maana sana katika uwasilishwaji wake katika neno au alama inayotumika.

Iwapo mfanyabiashara asipokuwa makini anaweza kujikuta akichanganya ujumbe kwa sababu mara nyingi lugha ya alama huwa na maana mbili tofauti kwa wateja tofauti  

Kwa upande mwingine, lugha ya sauti imekuwa kitendawili kwa watu wengi kushindwa kuwa chini ya mteja pale tofauti zinapotokea baina yao.

Maneno ya dhahabu kama samahani, nisamehe, karibu tena, jisikie upo salama, nikuhudumie kitu gani, na mengine mengi humfanya mteja ajisikie mwenye thamani. Wateja waliopata huduma bora na kupokewa kwa lugha nzuri huchangia kukua kwa brand ya biashara yako kwa kuwa siku utakuwa midomoni mwao.

Lugha nzuri unayotoa kwa wateja inachangia kwa kiwango kikubwa kupata wateja ambao huwa mabalozi wa bidhaa na huduma zako. Picha| Marketing Donut.

Vipi kuhusu mwenekano wa bidhaa?

Biashara nyingi zimekuwa zikijitofautisha kimwonekano kulingana na huduma wanazitoa na bidhaa wanazouza sokoni.

Mwonekano imekuwa sehemu ya kwanza inayoakisi aina ya watu na biashara husika. Kama wewe ni mama lishe au baba lishe tunategemea na tunajua mwonekano wako lazima uwe wa namna fulani.

Kwa bahati mbaya watu wamekuwa wakifanya biashara kimazoea kwa kuwa baadhi ya wafanyabishara wa chakula huwa ni wachafu, haewaleweki na hawafananii kabisa na chakula.

Mwonekano wa aina hii unakuondolea wateja kwa kuwa watakuwa wakihofia usafi wa chakula unachouza na watakuwa mabalozi wabaya wa brand yako huko nje.


Zinazohusiana:


Mtoa huduma, mafanikio ya kibiashara hayaji kutoka hewani yanajengwa na mtazamo, lugha nzuri na mwonekano. Kama biashara yako itasikika kwa kuwa na huduma bora hii ndiyo BRAND yako na huu ndiyo utambulisho wako wa kipekee sokoni.

Ukiwa na upekee kama huu utafanikiwa kuwa na thamani ya juu na soko lako litakuwa imara na kubwa na utawashinda washindani wako sokoni.

Lazima tutambue kuwa biashara zetu zinahitaji kiungo muhimu sana na moyo anaoitwa Huduma kwa wateja.

Tafiti zinaonesha kuwa ukimuhudumia mteja mmoja vibaya anao uwezo wa kuwaambia wateja wengine 10 wasije kununua bidhaa kwako na vilevile ukimuhudumia mteja mmoja vizuri anao uwezo wa kushawishi wateja wengine watatu waje kununua bidhaa yako.

Sasa  kazi ni kwako kuhudumia vizuri au kuhudumia vibaya. Tujenge brand zetu kwa misingi ya huduma imara na zenye mawasiliano chanya ya kibiashara na upendo.

Charles Nduku maarufu kama Mr Brand ni mkufunzi wa wajasiriamali katika masuala ya masoko na uhamasishaji wa kimaisha. Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana naye kupitia +255762918153 au baruapepe: mrbrandtz@gmail.com.