October 6, 2024

Namna wanafunzi wanavyoweza kutumia likizo zao ipasavyo

Ukifanya hayo utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutumia likizo yako vizuri kwa kufanya mambo yenye manufaa.

  • Panga ratiba ili kukamilisha mipango uliyojiwekea wakati wa likizo.
  • Fanya mazoezi na pata muda wa kuwa karibu na ndugu na marafiki.
  • Fanya biashara ndogo ndogo ili kujiongezea kipato. 

Likizo kwa wanafunzi wa ngazi zote ikiwemo shule za msingi, sekondari na hata chuoni hutumiwa zaidi kwa ajili ya mapumziko. Mapumziko huwa na lengo kuipa akili utulivu na kuiongezea uwezo tena wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. 

Likizo siyo tu kupumzika bali ni kujishughulisha na mambo mengine ambayo ni tofauti na masomo ili kuboresha maisha yako kwa namna tofauti. 

Kuna namna tofauti ambavyo wanafunzi wanaweza kutumia likizo zao katika kufanya mambo yenye manufaa. Fuata hatua hizi ili uitumie vizuri likizo yako:

Panga mikakati itakayokuongoza katika likizo yako

Hii ni hatua ya kwanza kabisa itakayokuongoza katika mambo unayotaka kufanya na kukuepusha kukaa kiholela bila ya kuwa na mipango ya nini utafanya katika muda wako wote wa likizo. 

Hii inasaidia kuweka mambo yako sawa kulingana na muda ulionao wa kukaa nyumbani kabla hujarudi katika masomo yako.

Kama unaweza andika na tengeneza orodha ya mambo utakayofanya na mikakati ya kuitekeleza. 

Panga ratiba inayotekelezeka 

Ratiba ni muhimu kwani inakupa muda wa kufanya na kukuongoza katika mambo unayotaka kuyafanya kwa wakati maalum. Ratiba ndiyo inakusaidia kutekeleza mipango uliyojiwekea wakati wa likizo.

Lazima ujue ni muda gani utawasaidia wazazi kukamilisha majukumu yao, muda wa kutembelea marafiki na muda utakaofanya majukumu yako mengine. Mambo muhimu unayoweza kufanya wakati wa likizo yako: 

Watembelee ndugu na marafiki

Ni moja ya vitu vya kuviwekea kipaumbele ukiwa katika kipindi cha likizo kujua hali za marafiki na ndugu ambao huenda hamkuonana kwa muda ili kuongeza ukaribu na upendo. 

Marafiki au ndugu ni watu muhimu wanaotusaidia kukamilisha furaha katika maisha yetu. 

Hivyo ni muhimu sana kutumia likizo vizuri ili kujijenga kwa namna moja au nyingine. Fanya mazoezi yanayokufaa ili kuuweka mwili katika msawazo unaotakiwa ili kujiandaa vema kwa kipindi kijacho cha masomo. Picha|Mtandao. 

Dhibiti matumizi ya pesa zako

Imekua ni kasumba mbaya kwa wanafunzi wengi waliopo shule, hata mimi nilivyokua shule kwamba katika pesa ya matumizi tunazopewa na wazazi wakati wa shule, tunatunza ili kutumia wakati wa likizo ambacho si kitu kibaya japo inabidi kuweka mpango mzuri kwajili ya matumizi ya hizo pesa.

Unaweza kutumia pesa zako kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinaweza kuongezea kipato na kujikimu kimaisha. 

 Jitolee katika kazi za kijamii

Unaweza kujitolea kwa kujumuika na watu wengine katika shughuli mbalimbali za kijamii. Pia kujitolea katika shughuli za kijamii kama kupanda miti, kuwahudumiwa watu wenye uhitaji ili kuboresha maisha yao. 

 Hii itakusaidia kujifunza kivitendo dhana ya maisha na jinsi watu wanavyohusiana na kushirikiana.


Zinazohusiana:


Soma vitabu na majarida

Likizo inaweza pia kuwa njia nzuri ya kusoma vitabu na majarida unayoyapenda ili kujiongezea maarifa. Angalia ni mambo gani unapenda katika maisha yako. 

Mfano unapenda ujasiriamali basi tafuta vitabu vya ujasiriamali ambavyo vitakuongezea maarifa na ujuzi utakaokamilisha ndoto za maisha yako utakapohitimu masomo. 

 Pumzika na fanya mazoezi 

Likizo ni wakati wa kutumia muda mwingi katika kupumzika na kufanya shughuli za kutujenga kimwili kwa sababu muda mwingi unapokua katika harakati za masomo unakosa muda wa kujijenga kimwili au kupumzika. 

Hivyo ni muhimu sana kutumia likizo vizuri ili kujijenga kwa namna moja au nyingine. Fanya mazoezi yanayokufaa ili kuuweka mwili katika msawazo unaotakiwa ili kujiandaa vema kwa kipindi kijacho cha masomo. 

Vivyo hivyo kwa wanafunzi wahitimu wa elimu ya juu, ni vizuri kutumia muda walionao katika kujishughulisha na mambo mbalimbali yenye manufaa ikiwemo biashara ili kukuza kipato chao.