Namna wenye magari ya gesi asilia wanavyookoa maelfu ya fedha Tanzania
Waliofunga mifumo ya gesi asilia kwenye magari yao wamefanikiwa kupunguza gharama za mafuta wanazotumia kila siku na kuwaletea ahueni ya maisha.
- Mpaka sasa magari yasiyopungua 300 yanatumia gesi asilia nchini.
- Wadau wa nishati wamesema teknolojia hiyo ikiwekewa mikakati itasaidia kulinda mazingira na kupunguza gharama za maisha.
- Serikali imesema inakusudia kuongeza uzalishaji na vituo vya gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini.
Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kila mahali duniani. Viongozi, wadau wa mazingira na hata wabunifu wanaoendelea kubuni njia mbadala za kuokoa mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi na kuendeleza vizazi.
Moja ya teknolojia inayoenea sasa ni matumizi ya nishati ya umeme na gesi asilia kuendesha vyombo vya usafiri ikiwemo magari.
Tayari kampuni kubwa duniani ikiwemo Tesla ya Marekani zinachangamkia matumizi ya umemejua kwenye magari na kuishawishi dunia kuachana na petroli na dizeli ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.
Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ya mwaka 2030 hasa lengo la 13 la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzuia ukataji miti, kulinda na kuendeleza maeneo yaliyohifadhiwa na kuhimiza matumizi ya nidhati jadidifu.
Lakini sasa inajielekeza katika matumizi ya nishati ya gesi asilia inayopatikana kwa wingi katika mikoa ya Kusini ikiwemo Mtwara na Lindi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani na kuendesha vyombo vya moto.
Gari ambalo limefungiwa mfumo wa gesi asilia linalopatikana katika karakana ya idara ya Uhandisi wa Mitambo ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT). Picha|Daniel Samso.
Matumizi ya gesi asilia kwenye magari yakoje Tanzania?
Katika kuongeza msukumo wa matumizi ya rasilimali ya gesi asilia inayopatikana kwa wingi nchini, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) inaendesha mradi wa ufungaji mfumo wa gesi asilia kwenye magari ya kawaida (Compressed Natural Gas-CNG) ili kuyawezesha kutembea barabarani kwa kutumia nishati hiyo.
Mfumo huo unaongezewa katika mfumo wa kawaida wa gari yanayotumia petroli. Nishati ya gesi asilia hutumika kama mbadala wa mafuta ya petroli.
Mhadhiri na Mratibu wa mradi huo kutoka DIT, Dk Esebi Nyari ameiambia www.nukta.co.tz kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2008 kwa majaribio ili kuiwezesha jamii ya Watanzania kutumia nishati rahisi na safi inayookoa gharama za maisha hasa kwa watumiaji wa vyombo vya moto.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 10 mradi huo ulikuwa unasuasua kutokana na changamoto ya fedha na upatikanaji wa gesi.
Lakini ulipata nguvu zaidi mwaka 2018 na sasa DIT inashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Viwango Tanzania kutekeleza mradi huo.
Kampuni nyingine ambazo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo ni Anric Gas Limited na Energo Tanzania Limited ambazo zimeungana na taasisi hizo za umma ili kufanikisha mradi huo kwa viwango vinavyotakiwa.
“Sasa kuna gesi ya uhakika kutoka Mtwara kupitia bomba la gesi ambalo linakuja mpaka Dar es Salaam kwa hiyo gesi inapatikana katika kituo cha Ubungo ambapo ni fursa ya kuongeza idadi ya magari yanayotumia mfumo huo,” anasema Dk Nyari.
Kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika jiji la Dar es Salaam ambalo linakabiliwa na adha kubwa ya foleni hasa kwa watumiaji wa vyombo vya moto. Foleni huongeza gharama za maisha kwa watumiaji wa vyombo vya moto kutokana na kutumia nishati kubwa ya mafuta wawapo barabarani.
- Maumivu: Bei ya mafuta zapaa
- Statoil yaja kivingine uchimbaji gesi Tanzania
- Mengi kuwekeza Sh68 bilioni uchimbaji wa mafuta, gesi Tanzania
Magari yanayotumia zaidi gesi asilia
Tangu mradi huo uanze, umefanikiwa kufunga mfumo wa gesi asilia katika magari yasiyopungua 300 huku mengi yakijihusisha na biashara ya abiria maarufu kama taxi. Miongoni mwa magari mengi yaliyobadilishwa ni aina ya Toyota IST ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania kutokana na unafuu katika uendeshaji wake.
“Tunaweka katika magari yote kuanzia madogo mpaka makubwa. Gari hizi za IST, Spacio mpaka gari kubwa za VT,” anasema Dk Nyari katika mazungumzo na www.nukta.co.tz yaliyofanyika leo Januari 14, 2020.
Kutokana na taxi kutumiwa na madereva kusafirisha watu ndani ya jiji, wamiliki wa magari hayo ambao wanatoa huduma ya usafiri kwa njia ya mtandao wakiwemo Uber na Bolt wanachangamkia fursa hiyo ili kupunguza gharama za uendeshaji magari.
“Uber nyingi zinatumia gesi asilia,” amesema Dk Nyari na kuongeza kuwa wameingia makubaliano na Uber ambapo benki zinatoa fedha kwa ajili ya madereva kufungiwa mifumo hiyo ya gesi asilia na wanakuwa wanalipa taratibu.
Magari yanayotumia gesi asilia yanapunguza gharama za mafuta kwa asilimia 60 ikizingatiwa kuwa bei ya gesi iko chini ukilinganisha na petroli ambapo humuwezesha dereva kutembea umbali mrefu kwa kutumia kiwango kidogo cha gesi.
Katika makala ya kesho tutaangazia kwa undani jinsi mifumo hiyo inavyofungwa kwenye magari na jinsi nishati hiyo inavyookoa gharama za mafuta na kuwaleta ahueni ya maisha wamiliki wa vyombo vya moto.