November 24, 2024

Nane mbaroni kwa wizi wa vifaa vya ujenzi daraja la Magufuli

Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu nane kwa kosa la kuiba vifaa vya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi (John Magufuli) zikiwemo nyaya.

  • Ni watu nane ambao wanatuhumiwa kuiba vifaa vya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi mkoani mwanaza.
  • Daraja hili la lililopewa jina la Magufuli litaunganisha mikoa ya Mwanza na Geita. 

Mwanza. Jeshi la  polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu nane kwa kosa la kuhujumu miundombinu ya ujenzi wa  daraja la Kigongo-Busisi (John Magufuli) baada ya kukamatwa wakiwa na vifaa  vya ujenzi  wa daraja hilo zikiwemo nyaya. 

Daraja hilo lililopewa jina la Hayati Rais Magufuli, lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 litakapokamilika mwaka 2023 litakaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Geita kwa kukatisha Ziwa Victoria.

Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza.

Kamanda wa polisi mkoani hapa Jumanne Muliro amesema  watuhumiwa hao walikamatwa Mei 4 mwaka huu wakiwa na gari aina ya Toyota Hiace lililokuwa limebeba vifaa hivyo. 

Amevitaja vifaa vilivyoibwa kuwa ni vyuma aina ya “H. beam 19”, nati kubwa 16 (bolt),  vifaa aina ya “Cutting  tot/ Welding Bubro 3”, mabomba mawili ya gesi na nyaya moja nyeusi. 

Katika mahojiano ya awali na dereva wa gari hilo alieleza vifaa hivyo alipewa na Joshua Wilison (43) mkazi wa Mbugani  ambaye ni fundi wa kuchomelea  vyuma. 

“Polisi walimkamata mtuhumiwa huyo na alieleza vifaa hivyo alivinunua kwa mafundi watatu wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi linaloendelea kujengwa,” amesema Kamanda Muliro. 

Watuhumiwa wote wamekamatwa na wanaendelea kufanyiwa uchunguzi. 


Soma zaidi: 


Daraja hilo litatatua kero ya miaka mingi iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.

Katika tukio jingine mtoto wa miaka mitatu mkazi wa kitongoji cha  Nyamuge wilayani Magu amefariki dunia baada ya kuliwa na fisi akiwa anacheza jirani na nyumbani kwao. 

Kamanda Muliro imesema tukio hilo limetokea Mei 6 mwaka huu saa 1:30  jioni. 

Kamanda Muliro anasema wakati tukio hilo  linatokea mama mzazi wa marehemu  alikuwa ndani anapika ghafla aliona mtoto anakokotwa na fisi  ndipo akaanza kupiga yowe kuomba msaada kwa majirani. 

“Wananchi walifuatilia michirizi ya damu hadi mlimani na kukuta mtoto  amefariki, “amesema