October 6, 2024

NBC ongezeni wigo wa kutoa huduma-Majaliwa

Awataka kusogeza huduma zao karibu na wananchi ili kuwavutia kutunza fedha zao katika hali ya usalama badala ya kuzihifadhi majumbani.

  • Awataka kusogeza huduma zao karibu na wananchi ili kuwavutia kutunza fedha zao katika hali ya usalama badala ya kuzihifadhi majumbani.
  • NBC yasema mwaka wa fedha uliopita wamefanikiwa kutengeneza faida na kwamba wanatarajia kutoa tena gawio kwa Serikali.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) iongeze wigo wa kutoa huduma ili kuwafikia wananchi wengi na kuongeza usalama wa pesa zao. 

Majaliwa ametoa wito huo leo (Februari 14, 2019)  wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha wananchi waongeze nguvu katika sekta ya kilimo, taasisi za fedha hazina budi kusogeza huduma zao karibu na wananchi ili waweze kutunza fedha zao katika hali ya usalama badala ya kuzihifadhi majumbani.

 “Ninatoa wito kwenu mpanue wigo katika utoaji wa huduma zake hapa nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhifadhi fedha zao katika eneo salama,” amesema Majaliwa.

Amesema benki  ya NBC imekuwa mstari wa mbele wa kuwawezesha wananchi kupitia mikopo kwa wajisiriamali wadogo ambayo inawawezesha kuongeza mitaji yao ya biashara mbalimbali.


Zinazohusiana: 


Kwa upande wake, Sabi ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara na mwaka wa fedha uliopita wamefanikiwa kutengeneza faida na kwamba wanatarajia kutoa tena gawio. 

Hata hivyo, hakutaja ni kiasi gani cha gawio kitatolewa, kwa sababu anasubiri uamuzi wa Bodi.

Mei 2017, NBC ilitoa gawio la Sh1.7 bilioni kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 za hisa kwenye benki hiyo. 

Pia amemkabidhi Waziri Mkuu hundi yenye thamani ya Sh11.2 milioni ambazo amesema zitasaidia katika ujenzi wa kituo cha polisi wilayani Ruangwa.