October 7, 2024

Nchi za SADC ziimarishe miundombinu kukuza viwanda-Mhandisi Kakoko

Miundombinu hiyo ni pamoja na reli, barabara, bandari na mawasiliano ili kukuza sekta ya viwanda katika mataifa hayo.

  • Miundombinu hiyo ni pamoja na  reli, barabara, bandari na mawasiliano ili kukuza sekta ya viwanda katika mataifa hayo. 
  • Hali hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na ajira kwa wananchi. 

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko amezitaka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuimarisha miundombinu ya reli, barabara, bandari pamoja na mawasiliano ili kukuza sekta ya viwanda katika mataifa hayo.

Mhandisi Kakoko amesema kwa sasa Tanzania imekuwa nchi ya mfano katika nchi za ukanda huo, kwa kuwa imekuwa kitovu cha usafirishaji wa bidhaa na malighafi mbalimbali katika nchi za SADC, hatua iliyotokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji. 

“Zipo Nchi chache ndani ya SADC ikiwemo Afrika Kusini ambazo tayari zimepata mafanikio makubwa katika miundombinu yake ikiwemo Bandari ya Durban, hivyo mkutano huu unakuwa chachu kwa Mataifa yote kuweza kubaini changamoto zilizopo ili kuhakikisha tunakuwa na mkakati wa pamoja wa kutuvusha hapatulipo” amesema Kakoko.

Alikuwa akizungumza jana (Agosti 6, 2019) wakati wa mjadala wa wataalam uliojadili umuhimu  ya sekta ya miundombinu katika  ujenzi wa uchumi wa viwanda katika nchi wananchama wa SADC,  katika Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za SADC yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi: Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC


Ili kufikia mafanikio hayo Serikali za SADC hazina budi kuweka msisitizo katika kuiwezesha sekta binafsi ikiwemo mashirika ya maendeleo ya kimataifa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya miundiombinu pasipo na kuweka masharti magumu kwa Serikali ili kuleta manufaa kwa wananchi walio wengi. 

Kwa mujibu wa Kakoko, TPA imeanza kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha kiwango cha ushindani na bandari nyingine kubwa barani Afrika na hivyo kuweza kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuwa kichocheo muhimu katika maisha ya wananchi.

Aidha, amesema miundombinu ya nchi za SADC kwa sasa si mizuri, ni  wajibu wa Mashirika na Taasisi za umma na binafsi kujitokeza ili kusaidia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu hiyo na hivyo kurahisisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Wiki ya Viwanda ambayo inawakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 inafanyika Jijini Dar es Salaam kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi 16 za SADC utakaofanyika Agosti 17 hadi 18 mwaka huu.