Ndege maalum kupambana na nzige wa jangwani Tanzania
Ni makundi ya nzige wa jangwani waliovamia mashamba ya wakulima na malisho ya mifugo katika Wilaya za Simanjiro na Longido.
- Serikali imeanza kutumia ndege kunyunyizia viuatilifu (sumu) ili kuwaangamiza wadudu hao.
- Ni makundi ya nzige wa jangwani waliovamia maeneo ya Wilaya za Simanjiro na Longido.
Dar es Salaam. Kufuatia uvamizi wa makundi ya nzige wa jangwani katika maeneo ya Wilaya za Simanjiro na Longido na kuhatarisha ustawi wa mazao na malisho ya mifugo kwenye maeneo hayo, Serikali imeanza kutumia ndege kunyunyizia viuatilifu (sumu) ili kuwaangamiza wadudu hao.
Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa kuanzia leo ndege maalum itafanya kazi kupulizia viuatilifu kuua nzige hao ambao wamekuwa wakiharibu mazao ya wakulima.
“Kuanzia kesho (Februari 22, 2020) ndege maalum itaanza kazi kupulizia sumu kuua nzige waliovamia maeneo ya Longido na Simanjiro ili wasiendelee kusambaa na kusababisha maafa,” amesema Waziri Mkenda Februari 21 alipotembelea eneo la Wilaya ya Longido, kaskazini mwa Tanzania ambalo limevamiwa na nzige hao.
Waziri Mkenda amesema tayari wataalam wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu (TPRI) wapo wilayani Longido na Simanjiro wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake Dk Efrem Njau kwa kazi ya kudhibiti wadudu hao waharibifu wa mazao ya kilimo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutokuokota wala kula nzige watakaokuwa wameuwawa na viuatilifu (sumu) kwenye maeneo yote ambapo ndege hiyo itapita kwani viuatilifu hivyo vinaweza kuwa na madhara kwa binadamu.
“Wananchi wakiona nzige wameanguka chini wamekufa wasiwachukue au kula kwa kuwa wengi watakuwa wamekufa kwa sumu” amesisitiza Prof Mkenda.
Zinahusiana:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Nguvu ya uharibifu waliyonayo nzige waliovamia Kenya, Uganda
Prof. Mkenda amesema nzige wa jangwani wana athari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na malisho ya mifugo na kundi moja la nzige lina uwezo wa kuruka bila kutua kwa umbali wa kilometa 150 kwa siku.
Nzige hao wa jangwani ambao wana urefu wa kidole cha mwanadamu huruka kwa makundi makubwa makubwa wakitafuta lishe ambapo kundi moja la nzige linaweza kuwa na wastani wa nzige milioni 40 kwenye eneo la kilometa moja za mraba.
Wadudu hao wamekuwa wakishambulia ukanda wa Afrika Mashariki wenye nchi za Djibout, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Yemen.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zinazofaidika na ruzuku ya dharura ya dola za Marekani 1.5 milioni (Sh3.5 bilioni) iliyotolewa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kukabiliana na nzige ambao wanatishia maisha ya watu na uhaba wa chakula katika eneo hilo.