November 24, 2024

Ndege ya ATCL yabisha hodi Afrika Kusini

Shirika la Ndege la Tanzania leo imeanza rasmi safari zake kutoka Tanzania hadi katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa kutumia ndege aina ya Airbus 220-300.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema lengo la kuanzisha safari hizo ni kupunguza muda ambao abiria walikuwa wanatumia kufika katika nchi hiyo iliyopo kusini mwa bara la Afrika. Picha|Mtandao.


  • Shirika la Ndege la Tanzania leo imeanza rasmi safari zake kutoka Tanzania hadi katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini. 
  • Ndege aina ya Airbus 220-300 ya ATCL imeondoka leo saa 4:30 asubuhi na itafika Afrika Kusini saa 6:45 mchana.
  • Itaondoa changamoto ya abiria kuunganisha ndege mbili.

Dar es Salaam. Ndege aina ya Airbus 220-300 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) leo imeanza rasmi safari zake kutoka Tanzania hadi katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini. 

Ndege hiyo imeondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 4:30 asubuhi na inatarajiwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini mchana wa leo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema shirika hilo litakuwa linafanya za safari za Afrika Kusini mara nne kwa wiki ili kuwaondolea usumbufu abiria waliokuwa wanaunganisha safari.

Amesema abiria wanaoenda katika nchi hiyo wamekuwa wakipitia Nairobi-Kenya au Ethiopia lakini sasa watakua wanasafiri moja kwa moja. 

“Tunaomba watanzania watupe ushirikiano na kupenda vya kwetu, tumeanza safari za kwenda Afrika Kusini na baadaye tunakwenda China na India,” amesema Matindi wakati akizungumza na Wanahabari wakati wa uzinduzi wa safari hiyo leo jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa ATCL, kwa sasa abiria watalipa nauli ya dola za Marekani 299 sawa na Sh687,688 ambapo viwango vipya vya nauli vitatangazwa baada ya Julai 15 mwaka huu. 


Soma zaidi:


Huenda huo ni mwendelezo wa mpango wa shirika hilo kupanua huduma zake za ndani  na nje ya nchi ambapo kwa sasa linatoa huduma katika mikoa 10 ya Tanzania ikiwemo Kilimanjaro, Kagera, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Dodoma,Tabora na Shinyanga.

Pia inafanya safari za anga katika nchi nne za Burundi, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema lengo la kuanzisha safari hizo ni kupunguza muda ambao abiria walikuwa wanatumia kufika katika nchi hiyo iliyopo kusini mwa bara la Afrika. 

Amesema pia usafiri huo wa ndege za ATCL utasaidia kuimarisha uhusiano ya kidiplomasia na biashara na Afrika Kusini ambao umekuwepo kwa muda mrefu sasa. 

Aidha, Kwandikwa amebainisha kuwa wamejipanga vizuri kuwahudumia Watanzania kwa huduma bora za usafiri wa anga na kuwawezesha kuyafikia maeneo mbalimbali duniani. 

Hata hivyo, ATCL itakuwa na kibarua kigumu cha kuboresha huduma zake, ikizingatiwa kuwa inashindana na mashirika makubwa ya Kenya Airways na Ethiopia Airlines ambayo yametawala soko la usafiri wa anga Afrika. 

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya wateja wa shirika hilo kuhusu ucheleweshaji na kuahirishwa kwa safari mara kwa mara, lakini Serikali imesema tayari imetatua changamoto hiyo ya kiufundi ndani ya shirika hilo.