November 24, 2024

Neema yawashukia wafanyakazi wa shamba la mkonge Tanga

Ni baada ya Serikali kutatua kero zinazowakabili katika shamba la mkonge la Kigombe Estate lililopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

  • Ni wafanyakazi wa shamba la mkonge la Kigombe Estate lililopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
  • Serikali yafanikiwa kutatua kero zinazowakabili kiwandani hapo ikiwemo mishahara na mazingira duni ya kazi.
  • Chama cha wafanyakazi chatakiwa kuonana mara kwa mara na mwajiri wa kiwanda hicho ili kutafuta ufumbuzi wa kero za wafanyakazi. 

Dar es Salaam. Serikali imekitaka chama cha wafanyakazi wa shamba la mkonge la Kigombe Estate lililopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga kujenga tabia ya kukutana na mwajiri wa shamba hilo mara kwa mara ili kutatua changamoto za wafanyakazi ikiwemo zinazohusu mazingira ya kazi, mishahara na posho.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama  ametoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kikazi katika shamba hilo jana ambayo imelenga kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa Januari 21, 2021 alipotembelea shamba hilo la mkonge lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited.

Miongoni maagizo yaliyotolewa na Majaliwa ni kutatua migogoro yote iliyopo katika shamba hilo ili kuhakikisha mwajiri na waajiriwa wanapata haki zao.

“Mwajiri anawajibu wa kusikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi waliyonayo na kutafuta ufumbuzi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wake, mkifanya hivyo mtaongeza tija na ufanisi katika utendaji wa majukumu yenu,” amesema Waziri Mhagama.


Soma zaidi: 


Amewataka maafisa kazi kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi katika shamba hilo na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kusimamia michango ya wafanyakazi hao katika mfuko huo i na kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi kuhusu fao la upotevu wa ajira.

Aidha, ameigiza Mamlaka ya Maji Safi wilayani Muheza kupima maji yanayotumiwa na wafanyakazi hao ili waweze kupata maji safi na salama. 

“Pia amewataka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) pamoja na NIDA(Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa) kushughulika kwa karibu suala la vitambulisho vya uraia ili TRA waweze kuwapatia TIN(Namba ya mlipa kodi) namba wafanyakazi ambao walisimamishwa kazi kurejea sehemu zao za kazi katika shamba hilo,” imeeleza sehemu taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ziara hiyo.

Shamba hilo ni miongoni mwa mashamba ya mkonge yaliyopo nchini ambayo yamekuwa yakilima zao hilo ambalo linategemewa kutoa malighafi mbalimbali zikiwemo nyuzi za kutengenezea kamba.