July 8, 2024

NFRA yatakiwa kufanya biashara ya mazao ya kilimo

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kubuni njia muafaka ya kuongeza mapato kwa kuhifadhi nafaka zaidi na kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa koti la bluu) akiongea na watumishi wa NFRA Kanda ya Shinyanga wakati alipokagua ghala la hifadhi ya mahindi jana mjini Shinyanga. Picha|Wizara ya Kilimo.


  • Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kubuni njia muafaka za kuongeza mapato.
  • Watakakiwa kufanya biashara ya mazao ya kilimo.
  • Akiba ya chakula katika maghala ya NFRA yazidi kupungua. 

Dar es Salaam. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kubuni njia muafaka ya kuongeza mapato kwa kuhifadhi nafaka zaidi na kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya jana (Aprili 28, 2020) mkoani Shinyanga wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazofanywa na NFRA kanda ya Shinyanga.

“Kuanzia sasa nataka kuona NFRA inafanya kazi kwa kujitegemea zaidi bila kutegemea fedha za Serikali kwa kubuni mikakati ya kutumia uwepo wa vihenge vya kisasa na ghala vinavyojengwa na serikali hapa Shinyanga,” amesema Kusaya.

Amesema wakala huo unatakiwa kuongeza wigo wa mapato kwa kujihusisha na biashara ya mazao na kuacha kuitegemea Serikali kwa kila jambo.

“Tafuteni mbinu itakayoifanya NFRA mhifadhi nafaka nyingi zaidi kama mahindi, choroko, maharage, mpunga na ziada muweze kuuza na kupata fedha za kujiendesha kibiashara ikiwemo kutumia fursa ya mahitaji makubwa ya nafaka hususan chakula kwenye nchi za jirani na Tanzania” amesisitiza Kusaya.

Amesema kuwa Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa Sh15.24 bilioni wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kwa kujenga vihenge (silos) sita vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na ghala moja kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka katika eneo la Ibadakuli mkoani Shinyanga.

Mradi huo utawezesha uhifadhi wa mazao toka kwa wakulima kuongezeka toka tani 14,500 za sasa hadi tani 44,500 kwa mwaka utakapokamilika mwezi Juni mwaka huu.


Zinazohusiana:


Ikiwa NFRA itaweza kutekeleza agizo hilo inaweza kuongeza hifadhi yake ya chakula ikizingatiwa kuwa imekuwa ikipungua na kuongezeka kulingana na upatikanaji wa chakula.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Machi 2020 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa hadi mwezi Februari 2020 NFRA ilikuwa na akiba ya chakula tani 41,231 kutoka tani 85,525 ya kipindi kama hicho mwaka jana. 

Hata hivyo, tangu mwezi Septemba 2019 akiba hiyo imekuwa ikishuka mfululizo.  

Ripoti ya BoT imeeleza kuwa kupungua kwa akiba ya chakula mwezi Februari 2020 kulisababishwa na NFRA kuuza tani 2,366 za mahindi kwa wafanyabiashara binafsi, Mpango wa Chakula wa Dunia (WFP) na Idara ya Magereza.

“Hii ilisababisha akiba ya chakula kilichokuwepo katika ghala la NFRA kufikia tani 41,231 mwezi Februari 2020 kutoka tani 43,597 za mwezi Januari 2020,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.