July 8, 2024

Nini kimeiipata mikoa ya Mara na Mjini Magharibi?

Mjini Magharibi imeingiza shule nne huku Mara ikiingiza shule tatu za mwisho katiya shule 10 za mwisho kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita.

  • Mjini Magharibi imeingiza shule nne za mwisho katika ya shule 10.
  • Mara nayo imeingiza shule tatu. 
  • Shule zote za mwisho mwaka 2018 zimekwepa mtego kurudi katika orodha hiyo ya shule 10 mwisho.

Dar es Salaam. Vigogo wanaosimamia elimu katika mikoa ya Mjini Magharibi na Mara huenda wasitamani kuona mara kwa mara jedwali linaloonyesha shule 10 za mwisho katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu. 

Shule saba kati ya 10 kutoka mikoa hiyo zimeingia Katika jedwali hilo ambalo hakuna shule hupenda kuingia na kuifanya kuwa mikoa yenye shule nyingi katika orodha hiyo ya shule za mwisho nchini.

Katika matokeo ya mtihani ya kidato cha sita mwaka 2019 yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Mjini Magharibi uliopo visiwani Zanzibar umeingiza shule nne katika shule 10 za mwisho ukichuana na Mara wa Tanzania Bara ulioingiza shule tatu.

Katibu Mtendaji wa Necta  Dk Charles Msonde aliwaambia wanahabari  jana (Julai 11, 2019) kuwa shule 10 zilizofanya vibaya mwaka huu ni Nyamunga (Mara), Hail Selessie (Mjini Magharibi), Tumekuja (Mjini Magharibi), na Bumangi (Mara). 

Shule nyingine zilizoshika mkia ni Buturi (Mara), Mpendae (Mjini Magharibi), Eckernforde (Tanga), Nsimbo (Katavi), Mondo (Dodoma) na Kiembesamaki ‘A’ Islmamic (Mjini Magharibi).

Katika matokeo hayo Mkoa wa Mjini Magharibi unaongoza kwa kuingiza shule nne kati ya shule 10 za mwisho ukifuatiwa na mkoa wa Mara uliongiza shule tatu  huku shule tatu zilizosalia zimetoka katika mikoa ya Tanga, Katavi na Dodoma.


Soma zaidi: 


Uchambuzi uliofaywa na mtandao wa habari wa nukta umebaini kuwa shule zote zilizo ingia kwenye orodha ya shule 10  za mwisho mwaka 2018 zimetoboa kwa kutoingia katika orodha hiyo mwaka 2019.

Miongoni mwa shule ambayo haijaingia katika orodha hiyo mwaka huu ni Ben Bella ya Mjini Magharibi. Shule hiyo kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita (2016-2018) haikutoka kwenye orodha hiyo ya shule za mwisho. 

Lakini mwaka huu imejitoa kwenye kundi hilo, licha kuwa matokeo yake siyo kuridhisha sana ikizingatiwa kuwa haina hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la kwanza na waliobaki wameangukia katika madaraja ya III,IV na O. 

Ni changamoto kwa shule hiyo kongwe na shule zingine za visiwani Zanzibar ambazo zimefanya vibaya katika matokeo ya mwaka huu, kuongeza juhudi katika ufundishaji kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa sahihi yatakayowawezesha kujibu mtihani mwaka 2020. 

Nyongeza na Daniel Samson