Njia mbadala kuwapaisha wanawake na fursa za mafunzo mtandaoni
Ni pamoja na kutumia mitandao ya kijamii, kuchangia mijadala katika majukwaa mtandaoni na kufuatilia tovuti zinazotangaza fursa za mafunzo.
- Ni pamoja na kutumia mitandao ya kijamii, kuchangia mijadala katika majukwaa mtandaoni na kufuatilia tovuti zinazotangaza fursa za mafunzo.
- Hakikisha unatambua mashirika na taasisi zinazotoa fursa kwa wanawake ili uweze kujua mbinu na vigezo za kuzipata.
- Ni wakati wa wanawake kuchangamka na kuacha kusubiri kuletewa fursa mkononi.
Dar es Salaam. Kila siku fursa za elimu kwa wanawake zinazidi kuongezeka ili kuwajengea uwezo wa kufika mbali, kujiimarisha kiuchumi na kuwa na mchango katika maendeleo ya jamii inayowazunguka.
Mashirika na taasisi mbalimbali duniani zinaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kutoa fursa sawa za elimu huku kipaumbele kikiwa kuwapa wanawake mafunzo na udhamini wa masomo na kozi mbalimbali zinazolenga kuwaongezea ujuzi na maarifa yanayohitajika katika soko la ushindani wa ajira.
Lakini fursa hizo na zingine haziwezi kuwafikia wanawake ikiwa hawana nyenzo muhimu za kupata taarifa.
Nukta tunakuletea njia za kutambua fursa za masomo kwa kutumia simu yako ya ‘smartphone’ zitakazokusaidia kufikia malengo yako ya kuelemika kwa njia mbalimbali.
Jiunge na mitandao ya kijamii
Hii ni kutokana na mashirika mengi yanayotoa huduma za udhamini wa masomo au mafunzo hutangaza kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na Twitter. Huko utakutana na viunganishi vya tovuti zilizosheheni taarifa mbalimbali.
Hapa cha kuzingatia ni lugha hasa kingereza kwasababu fursa nyingi zinapatikana nje ya nchi, hivyo hakikisha unajinoa vizuri katika lugha ili kuendana na kila kinachojiri ulimwenguni.
Hivyo kama unapenda kujiendeleza kimasomo au kupata mafunzo inatakiwa ujiongeze kwa kuzifuata akaunti ambazo unaona kabisa zinatoa fursa kwa kitu unachopenda kufanya.
Kama wewe ni mjasiriamali wa teknolojia basi fuata kurasa zinafanya masuala ya teknolojia na biashara.
Hata hivyo, si rahisi kupata nafasi kutokana na ushindani uliopo ila hakikisha unatumia uwezo wako kadri uwezavyo kuomba nafasi nyingi bila kuchoka.
Mitandao ya kijamii ni njia mojawapo ya kunufaika na fursa za elimu na mafunzo mbalimbali yanayoendelea duniani. Picha|Daniel Samson.
Tafuta tovuti zinazotoa matangazo ya fursa za masomo
Tumia simu yako vizuri tafuta tovuti kama Opportunities for Africans ambayo mara nyingi hutangaza fursa mbalimbali za mafunzo na masomo kwa waafrika.
Hivyo unaweza kutembelea mara kwa mara itakusaidia kujua ni fursa gani zimetangazwa kujua sifa zinazohitajika ili uweze kushiriki.
Jiongeze kwa kutafuta zingine, kwani baadhi ya tovuti hazipatikani kirahisi mpaka utakapojua unataka kujifunza nini.
Soma zaidi: Namna habari za mtandaoni zinavyoweza kubadili maisha
Jiunge na kozi za bure zinazotolewa mtandaoni
Hapa unatakiwa kutafuta kozi zitakazo kuongezea ujuzi, kama wewe ni mwanafunzi, mjasiriamali, mfanyakazi au mbunifu na unataka mafunzo zaidi basi kila unapoona fursa ya kozi yoyote jitahidi kuomba.
Zipo kozi au progrmu za mafunzo zinazotolewa bila malipo kinachotakiwa ni kutoa muda wako na bando la intaneti.
Hakikisha utakachosomea kinaongeza thamani katika shughuli zako ili usipoteze muda wa kusoma vitu visivyoendana na maslahi yako au visivyokuwa na manufaa baadaye.
Fursa utazipata ukiwa mdadisi wa taarifa zinazotolewa na tovuti mbalimbali. Picha|Daniel Samson.
Shiriki mijadala mtandaoni
Jifunze kuchangia mada zinazokuhusu katika mitandao ya kijamii. Hii itakufanya ufahamike na watu wenye mawazo sawa na wewe. Wanaweza kuwa ni ufunguo wa fursa zaidi ambazo usingeweza kuzipata kama ungekaa kimya.
Katika kushiriki mijadala hiyo, chagua yenye faida kwako inayoweza kukupeleka mbali na kukuongezea wigo wa marafiki wenye manufaa katika maisha yako.
Fursa hizo zitakuwa chachu ya kukua na kufanikiwa katika eneo unalofanyia kazi. Pia zitakuunganisha na watu mbalimbali duniani wenye ujuzi na maarifa. Kwa wanaopenda kutembea basi safari hazitakatika kwako na hutaacha kushuhudia mandhari nzuri ya dunia.