October 6, 2024

NMB yawekeza Sh1 bilioni huduma za jamii Tanzania

Sekta zinazofaidika na uwekezaji huo ni pamoja na afya na elimu.

  • Sekta zinazofaidika na uwekezaji huo ni pamoja na afya na elimu. 
  • Inatekeleza programu ya WAJIBU kuwanoa wanafunzi kwa elimu ya fedha. 
  • Yatoa vifaa vyenye thamani Sh25 milioni kwa zahanati ya Nandagala mkoa wa Lindi. 

Dar es Salaam. Benki ya NMB imesema imetenga zaidi ya Sh1 bilioni zitakazotumika katika uwekezaji wa shughuli za kijamii ikiwemo kuboresha sekta ya elimu na afya kwa wananchi wa Tanzania. 

Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali katika benki hiyo, Vicky Bishubo amesema kipaumbele cha benki hiyo kila mara ni kutatua changamoto za afya na elimu kwani sekta hizo ni nguzo kuu ya maendeleo kwa Taifa lolote duniani. 

“Mpaka ninavyoongea leo, tayari tumetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh600 millioni kwa mwaka huu wa 2019 tu,” amesema Bishubo jana (Julai 28, 2019) wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh25 milioni katika zahanati ya Nandagala, wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi. 

Amesema fedha hizo ni sehemu ya Sh1 bilioni walizotenga kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu.

NMB pia inatekeleza programu ya ‘Jifunze, Jipange na Wajibika’ (WAJIBU) ambayo mpaka sasa imeshawafikia vijana wasiopungua 42,000 katika shule za msingi na sekondari kwa kuwapa elimu ya fedha na kujifunza kuweka akiba katika umri mdogo. 

“NMB imekuwa ikiwawezesha vijana kupata elimu ya fedha katika shule za msingi na sekondari Tanzania. Elimu hii ya fedha kwa vijana hutolewa na wafanyakazi wetu wa benki kwenye shule zilizopo karibu na benki ikilenga kuwafundisha vijana umuhimu wa kuweka akiba na mipango kwa ajili ya maendeleo yao na kukidhi mahitaji ya muhimu,” amesema Bishubo. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, vifaa vilivyotolewa na NMB kwa zahanati ya Nandagala ni fremu 46 za madirisha ya ‘alminium’ na vioo vyake, milango 18, mabati 56, misumari na mbao, kompyuta 10, madaftari 4,050 vyote vikiwa na thamani ya Sh25 milioni. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa amesema mchango uliotolewa unamaanisha kazi ya kukamilisha jengo la wodi ya wagonjwa na vyumba vya madaktari katika zahanati hiyo ni lazima ifanyike haraka.

“Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NMB kwa msaada huu mkubwa. Hii maana yake ni kwamba ni lazima tuharakishe kukamilisha jengo hili ili tuanze kutoa huduma kwa wananchi wa Nandagala na wa vijiji vya jirani,” amesema Majaliwa na kuongeza kuwa,

“Tulianza na ujenzi wa zahanati kisha tukajenga jengo la upasuaji lenye wodi mbili. Moja ya wanaume na nyingine ya wanawake ambazo kila moja ina uwezo wa kulaza wagonjwa 20 kwa wakati mmoja.”

Amesema jengo hilo jipya likikamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 60 huku akiwataka wakazi hao wafikirie uwezekano wa kujenga wodi nyingine pamoja na jiko ili wagonjwa watakaokuwa wanalazwa hapo, wapate mahali pa kupikiwa chakula.