November 24, 2024

Nukta Africa yazindua maabara ya mafunzo ya aina yake Tanzania

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta imezindua maabara ya mafunzo ambayo ni ya kwanza kumilikiwa na kampuni ya kibiashara Tanzania itakayokuwa inatoa mafunzo yatakayosaidia kuikuza tasnia ya habari nchini.

  • Ni maabara ya kwanza kumilikiwa na kampuni binafsi nchini.
  • Maabara hiyo imelenga kutoa nafasi kwa watu kufanya kazi zao kwa ufasaha na kuchangia jitihada za kuzalisha wanahabari walio bora.

Dar es Salaam. Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta imezindua maabara ya mafunzo ambayo ni ya kwanza kumilikiwa na kampuni ya kibiashara Tanzania itakayokuwa inatoa mafunzo yatakayosaidia kuikuza tasnia ya habari nchini.

Maabara hiyo ya Nukta Lab iliyopo ghorofa ya 4, jengo la Dabe, mkabala na soko la Mwananyamala  jijini Dar es Salaam, itakuwa kiungo muhimu kwa wanahabari, watafiti, wanafunzi na wadau wa habari kujifunza ujuzi na teknolojia mpya zinazohitajika katika tasnia ya habari. 

Wataalam na wakufunzi wa Nukta Lab ambayo imezinduliwa leo Machi 5, 2021, watajikita zaidi katika kutoa mafunzo yanayohusu uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji habari, zana na teknolojia zinazohitajika katika vyombo vya habari hasa vile vya mtandaoni na vinavyochipukia.

Siyo tu itatumika kama jukwaa la kujifunza bali ni sehemu sahihi kwa ajili ya watu wenye fikra, wanaoependa kujisomea na kuifanya tasnia ya habari Tanzania kuwa yenye ushindani katika utengenezaji wa maudhui bora yenye viwango vya kimataifa. 

Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Biashara wa Nukta Africa, Daniel Mwingira amesema maabara hiyo ina uwezo wa kuchukua watu 10 mpaka 15 kwa wakati mmoja katika mazingira tulivu na rafiki kumuwezesha mtu kutimiza maelengo yake.

Mwingira ambaye ndiye msimamizi wa Nukta Lab amesema maabara hiyo ina huduma zote za msingi ikiwemo intaneti yenye kasi nzuri, kompyuta za kisasa, runinga ya kidijitali na viyoyozi kuendana na mahitaji ya kila mtumiaji. 

Maabara hiyo ya aina yake, kwa mujibu wa mtaalam huyo, pia ina huduma muhimu za teknolojia ikiwemo mifumo ya kidijitali iliyounganishwa na programu na zana ambazo zinamrahisishia mtumiaji kukamilisha mafunzo na shughuli zake kwa wakati.

“Malengo yetu ni makubwa katika kuwekezwa katika mfumo wa kijigitali. Kuna vifaa vyote muhimu kwa ajili ya mafunzo.Maabara inaweza kuchukua watu 10 mpaka 15 huku watu takribani 9 kuweza tumia kompyuta za lab kwa ajili ya kujifunzia.” Amesema Mwingira. 

Aidha, Nukta Lab inatumika kama ukumbi wa mikutano, vikao, warsha na semina zinazoratibiwa na mashairika, kampuni na taasisi mbalimbali. Uongozi wa maabara hiyo umefungua milango kwa watu wanahitaji kuitumia na kuahidi kuwa watatoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya mteja. 

“Tunatoa wito kwa wadau wetu kuchangamkia fursa hii, tuna imani itakua mwanzo wa mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari nchini,” Maphosa Banduka, Mkuu wa fedha na utawala, Nukta Africa amesema.

Banduka ameongeza kwa kusema, katika sekta ya habari, wanatamani kuona waandishi wanachapisha habari zenye kuleta mabadiliko katika jamii.

“Tunatamani kuona waandishi wanaleta habari zenye kuleta mchango chanya na kutatua matatizo mbalimabali katika jamii zetu wakitumia takwimu ili kuboresha maisha ya watu,” amesema Banduka.


Soma zaidi:


Nukta Lab ni bidhaa mpya kabisa ambayo inamilikiwa na Nukta Africa inayofanya kazi ya kuboresha maisha ya watu kwa kutumia takwimu na maudhui ya mtandaoni.

Kampuni hiyo pia inamiliki tovuti ya habari (www.nukta.co.tz), inatoa huduma za kutengeneza infografia, ushauri wa jinsi ya kutumia mifumo ya teknolojia, data (takwimu) na mbinu bora za kuboresha utendaji wa vyombo vya habari.

Kwa taarifa zaidi, unaweza kuwasiliana nasi kwa namba: +255 677 088 088 au kwa barua pepe: info@nukta.co.tz au kwa mitandao yetu ya kijamii ya Facebook, Twitter na LinkedIn @Nukta Africa na @nuktaafrica kwa Instagram.