October 8, 2024

Nyota inavyotumika kutofautisha hadhi za hoteli duniani

Muhimu ni kujua kuwa, nyota katika biashara ya hoteli duniani zina maana yake na zaidi, nyota hizo huonyesha huduma ambazo zinatolewa katika hoteli husika.

  • Nyota za hoteli ni kiwango cha ubora kwenye hoteli.
  • Kiwango cha juu ni nyota tano huku cha chini kikiwa ni nyota moja.
  • Huduma zitolewazo kwenye kila hoteli, hutegemea kiwango cha nyota za hotelli hiyo.

Dar es Salaam. Huenda umewahi safiri kwenda sehemu na baada ya kuulizia hoteli nzuri, swali la “nyota ngapi” lilifuata. Bila kujua unachojibu, huenda jibu lako lilikua “yoyote” na kujikuta uko katika hoteli nje ya matarajio yako.

Muhimu ni kujua kuwa, nyota katika biashara ya hoteli duniani zina maana yake na zaidi, nyota hizo huonyesha huduma ambazo zinatolewa katika hoteli husika.

Hakika unahitaji kufahamu maana ya nyota hizo na huu ndio uchambuzi wake. Hadhi za hoteli huanzia nyota moja hadi nyota tano ambayo ni hoteli ya hadhi ya juu kabisa duniani au gharama zake ziko juu. 

Hoteli za nyota moja

Hiki ndicho kiwango kidogo zaidi kwenye viwango vya hoteli. Ukiingia katika hoteli za nyota moja, hutakiwi kuwa na matarajio makubwa juu ya huduma zitolewazo. 

Haina maana kuwa hoteli hizi ni chafu na hazina matunzo, La hasha! Ina maana utapata sehemu ya kulala na huduma muhimu, hilo ndilo kubwa zaidi. Mfano wa hoteli hizi kwa jijini Dar es Salaam ni Stay Inn Hotel iliyopo karibu na barabara ya Msimbazi, mtaa wa Swahili.

Nyota mbili nazo maana yake hii hapa

Kama ilivyo kwa hoteli za nyota moja, nyumba hizi ambazo ni makazi ya muda mfupi zinakuja na bei ambayo ni rafiki kwa mtu mwenye bajeti ya kawaida. 

Ukiwa na pesa kuanzia Sh80,000 unaweza kupata chumba kwenye hoteli zenye kiwango hiki.

Mara chache, hoteli hizi huwa na huduma za ziada kama usafiri (unaomilikiwa na hoteli) wa kukusafirisha kwenda uwanja wa ndege na kadharika. 

Mfano wa hoteli hizi jijini Dar es Salaam ni Kiceck hotel iliyopo barabara ya uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam na Mesuma hotel iliyopo Makumbusho.

Siyo kwamba zitakuwa hoteli chafu. La hasha! Ina maana utapata sehemu ya kulala na huduma muhimu, Picha| booking.com.

Vipi hoteli za nyota tatu. Mambo yakoje?

Hoteli hizi ambazo mambo huanza kuwa afadhali hasa katika huduma na vitu vya ziada ikiwemo chakula na kadhalika.

Mfano wa hoteli hizi ni hoteli ya Mediterano na Regency Park hotel za jijini Dar es Salaam.

Cha ziada unachoweza kupata kwenye hoteli hizi ni pamoja na bwawa la kuogelea, sehemu ya kufanyia mazoezi na hata sehemu ya kuegesha gari lako binafsi.

Hoteli za nyota nne

Unapoongelea hoteli za nyota nne, kwa Dar es Salaam unaongelea Ramada Resort, White Sand hotel zilizopo Kunduchi na zinginezo nyingi kama Double Tree na Landmark ya Mbezi beach.

Bwawa la kuogelea, sehemu ya mazoezi, mgahawa na huduma za kisasa ni kati ya vitu unavyoweza kuvipata katika  hoteli hizi ambazo zinakuhitaji uwe na mpunga kidogo.

Mfano, kama ukifanya “booking” leo, katika hoteli za nyota nne kwa kutaka kutumia usiku mmoja, unahitaji walau fedha kuanzia Sh150,000 hadi Sh461,000 japo unaweza kupata chini ya hapo ukifanya utafiti.

Bwawa la kuogelea, sehemu ya mazoezi, mgahawa na huduma za kisasa ni kati ya vitu unavyoweza kuvipata katika  hoteli hizi ambazo zinakuhitaji uwe na mpunga kidogo. Picha| Trip advisor.

Na hii ndiyo maana ya hoteli za nyota tano

Kiwango hiki ni cha juu zaidi kwenye viwango vya hoteli.

Popote unapoenda, hoteli za kiwango hiki zitahitaji pochi yako iwe na afya ili kuweza kumudu kutumia muda wako hapo.

Kwa jijini Dar es Salaam, hoteli hizi zinawakilishwa na Johari Rotana iliyopo Posta ambayo kama ukiweka “booking” kuutumia usiku wa leo hapo, itakuhitaji Sh507.542 endapo utafanya “booking” yako kwa njia ya mtandao.

Pia, hoteli kama Serena, Hyatt Regency na Sea Cliff zilizopo Dar es Salaam pia zinaingia katika kundi hili. 

Unahitaji sio chini ya Sh500,000 kwa usiku mmoja kuvinjari kwenye hoteli za aina hii.

Utakachokipata ni ubora katika kila huduma zilizopo mfano wa kitanda kikubwa, na mengine mengi.


Zinazohusiana


Kabla ya kuingia hotelini ni muhimu kufanya utafiti wa aina ya hoteli unayotaka kulingana na uwezo wako wa kiuchumi. Pia angalia huduma zinazotolewa katika hoteli husika kama zinakidhi matarajio yako.

Yote haya unaweza kuyafanya katika kiganja cha mikono yako kwakutumia simu ya mkononi. Unapenda kukaa katika hoteli ya nyota ngapi?