July 8, 2024

Ongezeko la vituo vya mafuta lachochea ushindani Tanzania

Idadi ya vituo vya mafuta ya magari Tanzania Bara imeongezeka kwa asilimia 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jambo linaloongeza ushindani kwa wafanyabiashara na kuwafaidisha zaidi wanunuzi.

  • Hadi kufikia Machi 31 mwaka huu Tanzania bara ilikuwa na vituo vya mafuta ya petroli 1,646 kutoka 1,500 vya Aprili 30, 2019.
  • Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo wenye vituo vingi zaidi Tanzania.
  • Ongezeko hilo limechochea ushindani wa biashara hiyo na kuwafaidisha zaidi wanunuzi.

Dar es Salaam. Idadi ya vituo vya mafuta ya magari Tanzania Bara imeongezeka kwa asilimia 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jambo linaloongeza ushindani kwa wafanyabiashara na kuwafaidisha zaidi wanunuzi. 

Mafuta hayo ambayo hujumuisha mafuta ya taa, dizeli, petroli imekuwa ni nishati muhimu inayotegemewa kuendesha vyombo vya moto yakiwemo magari na mitambo ya uzalishaji.

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amesema hadi kufikia Machi 31 mwaka huu Tanzania Bara ilikuwa na vituo vya mafuta 1,646 vikiwa vimeongezeka kutoka vituo 1,500 vilivyokuwepo hadi Aprili 30, 2019. 

Ongezeko hilo ni sawa na vituo 146 au asilimia 9.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kwa mujibu takwimu za Dk Kalemani katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha wa 2020/2021, asilimia 57.4 au sawa na kusema takriban vituo sita kati 10 viko katika mikoa 10 tu ya Tanzania Bara. Mikoa hiyo 10 kwa ujumla ina vituo 944. 

Majiji matano ya Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Arusha yamefanikiwa kuingia katika orodha hiyo isipokuwa jiji moja tu la Tanga ambako kuna kuna moja ya bandari ambaz hupokea pia shehena ya mafuta Tanzania.

Licha ya mikoa hiyo kuwa vinara wa vituo vingi vya mafuta, jiji la Dar es Salaam ndiyo limeshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na vituo vingi nchini. 

Hadi kufikia Machi 31, jiji hilo ambalo ndiyo kitovu cha shughuli za uchumi Tanzania lililikuwa na vituo 237 sawa na asilimia 14.4 ya vituo vyote vilivyorekodiwa kipindi hicho.

Vituo hivyo ambavyo wamiliki wa magari huingia kununua petroli na dizeli vimeongezeka kidogo kutoka 220 vilivyokuwepo Aprili 30, 2019.


Kunani Pwani?

Licha Mkoa wa Pwani kushika nafasi ya tatu kwa vituo vingi nchini, ndiyo mkoa pekee ambao idadi ya vituo vyake ilishuka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Vituo vya mkoa huo vimepungua kutoka 104 vilivyorekodiwa Aprili 30, 2019 hadi 102 Machi 31 mwaka huu.

Hotuba hiyo ya Wizara ya Nishati pia imeitaja mikoa 10 ambayo ina vituo vichache vya mafuta nchini ambapo Katavi ndiyo mkoa wenye vituo vichache kabisa Tanzania Bara.

Maskini Katavi!

Hadi Machi 31, Katavi ulikuwa na vituo 13 tu ikiwa ni pungufu zaidi ya mara 18 ya vile vilivyopo Dar es Salaam. 

Mikoa mingine yenye vituo vichache ni Rukwa yenye vituo 18, Simiyu (29), Singida (31), Songwe (33), Lindi (36) na Iringa yenye vituo 37.

Orodha hiyo pia ina mikoa ya Njombe yenye vituo 37, Ruvuma (38) na Tabora vituo 40. 


Zinazohusiana


Ushindani nao waongezeka

Ongezeko la vituo vya mafuta hasa katika majiji makubwa Tanzania unaelezwa na wachambuzi na wadau wa sekta hiyo kuwa linachochea ushindani wa biashara ya mafuta jambo ambalo huchangia uwepo wa bei nafuu kwa walaji. 

Muuza mafuta katika kituo cha kampuni ya Engen kilichopo Goba, Rose Mwamaja ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa ushindani umeongezeka lakini haujaathiri biashara yao kwa sababu wana wateja ambao lazima watanunua mafuta yao na siyo mtu mwingine.

“Ushindani ni kweli umeongezeka lakini brand (nembo ya kampuni ya mafuta) ndiyo itakuyokufanya uendelee kuwepo kwenye ushindani na kuuza zaidi ya wenzako kwa sababu ya ubora wa mafuta unayouza,” amesema Mwamaja.

Amesema utoaji huduma nzuri kwa mteja ikiwemo ukarimu, mazingira yanayovutia ya kituo yanasaidia wateja kuendelea kuwaamini na kununua mafuta yao.

Mei 5, 2020 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mwezi Mei 2020 ambapo yameshuka kwa viwango tofauti na kuwaletea ahueni wamiliki wa vyombo vya moto.

Katika bei hizo mpya, wateja wa rejareja wanaotumia mafuta yaliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam Sh219 wataokoa kwa petroli na Sh143 kwa dizelikila lita moja watakayonunua ikilinganishwa na bei zilizotumika mwezi uliotangulia wa Aprili.

Ongezeko la vituo vya mafuta linaongeza pia ushindani. Hata hivyo ubora wa mafuta na huduma nzuri kwa wateja vitasaidia baadhi ya kampuni kuhimili ushindani. Picha|Mtandao.

Licha ya kuwa bei elekezi ya petroli kwa lita moja jijini Dar es Salaam ni Sh1,868 lakini utafiti wa Nukta Habari umebaini baadhi ya vituo vya mafuta vinauza hadi Sh1,800 kwa lita huku baadhi ya wahudumu wakieleza kuwa hatua hiyo imelenga kuwavuta zaidi wateja kutokana na ushindani. 

Ushindani wa biashara hiyo ya mafuta unachagizwa pia na idadi ya watu waliopo katika eneo vilivyopo vituo hivyo.

“Ukitazama kama majiji ya Dar es Salaam na Arusha huko watu wengi ambao uchumi uko vizuri wanamiliki magari. Ni lazima watakuwa wanatumia mafuta, watayapata wapi? Ni kwa watu kujenga vituo kwa wingi ili wafaidike,” amesema John Mkenzi ambaye ni mmiliki wa daladala jijini Dar es Salaam.

Mkenzi ambaye hapo awali alikuwa akijihusisha na biashara ya magari, amesema pia urahisi wa upatikanaji wa mafuta ya petroli na dizeli nao unachangia kuwafaidisha wawekezaji wa biashara hiyo muhimu. 

Mtandao wa Future Learn wa Australia unaeleza kuwa miundombinu bora ya barabara na wingi watu katika mji au mkoa navyo ni kivutio cha uwekezaji wa vituo vya mafuta kwa sababu ya kuwepo kwa shughuli nyingi za uzalishaji zinazohitaji mafuta.