Ongezeni kasi ya kukusanya takwimu sahihi-UN
Umoja wa Mataifa (UN) umezitaka nchi wanachama wake ikiwemo Tanzania kuweka mifumo imara ya kukusanya takwimu sahihi na kwa wakati ili zisaidie katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.
- Umoja wa Mataifa (UN) umezitaka nchi wanachama wake ikiwemo Tanzania kuweka mifumo imara ya kukusanya takwimu sahihi na kwa wakati.
- Imesema takwimu sahihi na zinazozingatia wakati ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote.
- Zitasaidia kufanya maamuzi katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.
Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umezitaka nchi wanachama wake ikiwemo Tanzania kuweka mifumo imara ya kukusanya takwimu sahihi na kwa wakati ili zisaidie katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.
Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres amesema wakati nchi na mashirika yakijizatiti kutekeleza ajenda ya mwaka 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu, takwimu sahihi na zinazozingatia wakati ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote.
“Tunahitaji mabadiliko katika takwimu, tunahitaji kuimarisha uwezo wa ukusanyaji takwimu na kutumia teknolojia za kisasa, tunahitaji mchango na ujuzi wa wasimamizi wa takwimu na watumiaji na wasomi, sekta binafsi za vyama vya kiraia,” amesema Guaterres.
Guaterres amesema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya takwimu duniani ambayo huadhimishwa kila Oktoba 20, huku akisisitiza kuwa “uwekezaji sahihi unafanyika, vifaa vya teknolojia vipo, na sehemu mpya za kupata takwimu zinatumika na mbinu bunifu zinatumika kwa ajili ya kuhakikisha kila nchi inapata mifumo kamilifu ya taarifa wanazozihitaji kwa ajili ya kufikia maendeleo endelevu.”
Soma zaidi:
- Wanazuoni wamuenzi Prof Hirji, mtaalam wa takwimu za kitabibu
- Weledi, takwimu sekta ya nishati kuwatoa Wanahabari Tanzania
Siku ya takwimu duniani mwaka huu imeadhimishwa kwa kauli mbiu, “Takwimu bora, maisha bora.”
Amesema dunia inahitaji takwimu hasa vijijini kuhakikisha kuwa kila mtoto anafikia huduma ya elimu na takwimu za kimataifa za kufuatilia madhara jumla ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Takwimu sahihi ni muhimu kwa ajili ya kufanya maamuzi bora kwa watu wote katika jamii, na hii ilitambulika mwaka 2014 wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha masharti ya takwimu rasmi kama njia ya kufikisha taarifa kwa umma.
Umoja wa Mataifa umesema katika miaka 15 iliyopita, nchi nyingi zimepiga hatua katika kuimarisha uwezo wao wa kitaifa wa takwimu chini ya uongozi wa ofisi za kitaifa za takwimu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo umesema ufuatiliaji kwa ajili ya mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu unazua changamoto hata katika nchi zilizoendelea, jambo linalokwamisha utekelezaji wa malengo hayo kikamilifu.