October 6, 2024

PASS kuwawezesha vijana sekta ya kilimobiashara

Vijana watakaopata fursa ya kuingia kwenye atamizi za mafunzo hayo wanatakiwa wawe ni wahitimu wa shahada ya kwanza kutoka katika fani yoyote

  • Vijana kuchangamkia fursa ya kupata mafunzo ya kilimobiashara cha mbogamboga kuku,samaki na mbuzi.
  • Mafunzo hayo ni sehemu ya mchango kuelekea ujenzi wa uchumi wa viwanda. 
  • SUA, TALIRI kuratibu mafunzo hayo kwa miezi 12.

Dar es salaam.Shirika la Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo (PASS) limefungua milango kwa vijana kuchangamkia fursa ya kupata mafunzo ya kilimobiashara ili kukuza ujuzi na uzalishaji wa mazao na wanyama utakaowanufaisha kiuchumi.

Fursa zilizotolewa na PASS ni kujiunga katika mafunzo yatakayotolewa katika vituo atamizi vya kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa kuku, samaki na unenepashaji wa mbuzi vilivyopo wilaya ya Kongwa na Morogoro.

Meneja wa Kuendeleza Biashara kutoka PASS, Nelson Burton amesema vijana wanatakiwa kuchangamkia fursa kila zinapojitokeza hasa kwenye sekta ya kilimo ili kuwa sehemu ya uzalishaji mazao yenye viwango vya ubora.

“Tunaamini tutakapoweza kufanya atamizi ya vijana hao kila mwaka wataweza kuzalisha malighafi kutoka katika maeneo hayo manne ambayo yataweza kuongeza uzalishaji katika sekta ya viwanda,” amesema Burton.

Mafunzo hayo yataratibiwa na Kituo cha Uvumbuzi wa Kilimobiashara (AIC) kilichopo chini ya  PASS kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kampusi ya Morogoro kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa kuku na samaki; Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya  TALIRI (Tanzania Livestock Reserch Institute) iliyopo wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma kwa ajili ya unenepeshaji wa mbuzi.

Hata hivyo, vijana wenye nia ya kuingia kwenye mradi huo watalazimika kutoboa mifuko yao kwasababu wanatakiwa kujigharamia pesa za malazi na chakula katika kipindi chote cha miezi 12 ya mafunzo hayo, ikiwa ni sehemu ya kupima utayari wao katika kuzisaka fursa zinazoweza kuwatoa kwenye umaskini na ukosefu wa ajira.


Yanayokuhusu: Rasmi:Tabora ndiyo makao ‘makuu ya kuku wa kienyeji Tanzania’


Pia sifa nyingine ni kuwa mhitimu wa shahada ya kwanza kutoka katika fani yoyote, kuandika andiko bora la mradi wa kilimobiashara. Mradi huo una nafasi zisizopungua 50 za vijana wenye nia ya kutoka kimaisha ambapo wakipita vihunzi vyote watapata mafunzo, vifaa, ushauri wa kibiashara pamoja na miundombinu ya kuendesha miradi yao. 

“Wale watakoshinda katika mradi wa kufuga mbuzi watapelekwa Kongwa katika kituo cha TALIRI kwa ajili ya kufanyiwa atamizi huko.’’ amesema Burton na kubainisha kuwa lengo ni kukuza ubunifu kwa vijana, “’Watasaidiwa pia kutafutiwa masoko  ya bidhaa zao pamoja na ardhi baada ya kuondoka katika maeneo ya atamizi hizo mbili kwa wale wasio na ardhi.”