October 6, 2024

Pesa zilizokamatwa Kenya kujenga barabara Pori la Akiba la Selous

Barabara hiyo itaanzia Fuga mkoani Pwani itakayounganisha hifadhi mpya ya Taifa inayotarajiwa kuanzishwa katika Pori hilo.

  • Barabara hiyo itaanzia Fuga mkoani Pwani itakayounganisha hifadhi mpya ya Taifa inayotarajiwa kuanzishwa katika Pori hilo.
  • Itakuwa na urefu wa kilomita 60 na kufungua fursa mbalimbali za utalii.
  • Amesema dhahabu na fedha hizo zilizorudishwa zina thamani ya takribani Sh5 bilioni. 

Dar es Salaam. Serikali imesema dhahabu na fedha zilizorudishwa kutoka Kenya zitatumika kujenga barabara ya Fuga mkoani Pwani itakayounganisha hifadhi mpya ya Taifa inayotarajiwa kuanzishwa katika Pori la Akiba la Selous. 

Rais John Magufuli alipokea kilo 35.34 ya dhahabu na fedha zilizokamatwa baada ya kutoroshwa na wahalifu waliovamia benki ya NBC tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro mwaka 2004. 

Zoezi la makabidhiano ya dhahabu na kiasi cha fedha kilichokamatwa yalifanyika Julai 24, 2019 baina ya maafisa wa Serikali ya Kenya na Tanzania na kushuhudiwa na Rais Magufuli aliyevisifu vyombo vya dola vya nchi hiyo jirani kwa kazi nzuri waliyoifanya. 

Akizungumza leo (Julai 26, 2019) wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kufua umeme kwenye Mto Rufiji mkoani Pwani, Rais Magufuli amesema dhahabu hiyo pamoja na fedha zilizorudishwa zinakadiliwa kufikia Sh5 bilioni zitatumika kujenga barabara hiyo yenye kilomita 60. 

“Na kwa sababu juzi juzi zimerudishwa dhahabu kutoka Kenya nimezipigia hesabu kidogo, zilirudishwa hela zaidi ya Sh500 milioni, zile dhahabu inawezekana nazo zikachukua kama Sh4 bilioni ukizijumlisha ni karibu Sh5 bilioni, zianze kutengeneza barabara ya lami hii kuanzia Fuga ni kilomita 60 kutoka hapa (Pori la akiba la Selous),” amesema Rais Magufuli.


Zinazohusiana:


Amesema barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu kwa shughuli za utalii zitakazokuwa zinafanyika katika hifadhi mpya ya Taifa inayotarajiwa kupatikana baada ya kugawanywa kwa Pori la Akiba lenye ukubwa wa kilomita za mraba 54,600.

“Watu watakuwa wanatoka Dar es Salaam kwa treni wanatelemka Fuga, wakishatelemka Fuga wanaikuta barabara ya lami wanakuja kufanya utalii hapa,” amesema Rais na kuitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kujiandaa kwa shughuli hiyo. 

Amesema uamuzi wa kujenga barabara hiyo umezingatia umbali wa kufika Pori la Akiba la Selous ambapo unajengwa mradi wa kufua umeme wa megawati 2,115 kwenye mto Rufiji. 

“Kutoka hapa kwenda barabara ya Rufiji ya lami ni kilomita 198. Kutoka hapa ukizungukia Ubenazomozi kuna kilomita 330 bado hujaongeza za kutelemka huku. Kwahiyo angalau tujaribu hii short cut (fupi) hapa ya kilometa 60 mpaka Fuga tuanze kutengeneza polepole,” amesema.

Huenda ujenzi wa barabara hiyo ukafungua fursa mbalimbali kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la mto Rufiji.