July 8, 2024

Polisi waeleza Mbowe alivyoshambuliwa Dodoma

Ni kiongozi wa pili wa juu wa Chadema kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati wakiwasili kwenye makazi yao.

  • Anaendelea na matibabu katika moja ya hospitali mkoani humo.
  • Chadema mbioni kumhamishia Dar es Salaam.
  • Ni kiongozi wa pili wa juu wa Chadema kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati wakiwasili kwenye makazi yao. 

Dar es Salaam. Jeshi la polisi limeeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe alishambuliwa na watu watatu wasiojulikana na kumjeruhi kwa kumpiga mateke, dakika chache baada kuwasili nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumanne jijini Dodoma.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Giles Muroto amewaambia wanahabari kuwa kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani alikutwa na madhira hayo majira ya Saa 6:45 usiku baada ya kuteremka kwenye gari lake.

“Baada ya kushuka kwenye gari nyumbani kwake Area D inadaiwa alikutana na watu watatu waliokuwa wamevaa majaketi. Watu hao walimshambulia kwa kumpiga mateke na hasa mguu wake wa kulia,” amesema Muroto.

Baada ya shambulizi hilo, Muroto amesema kiongozi huyo aliwahishwa katika hospitali Ntyuka DMCT jijini hapo kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Muroto amesema wanafanya uchunguzi wa tukio hilo na kwamba “hawataacha chochote kuupata ukweli”.

“Tukio hili ni tukio kama mengine na linachunguzwa na polisi, lisitumike vibaya. Lisitumike kisiasa au kwa njia yeyote ya kujiongezea umaarufu,” amesema huku akiongeza “eneo lile lina walinzi  na majirani tutapata ukweli kuhusu tukio hilo.”


Soma zaidi: 


Hii ni mara ya pili ndani ya miaka mitatu kwa kiongozi wa juu wa Chadema kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea katika makazi yake jijini Dodoma.

Septemba 2017 Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu alishambuliwa na risasi na kumuachia majeraha lukuki mwilini kiasi cha kumlazimisha kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Uongozi wa Chadema umesema kuwa kwa kushirikiana na madaktari upo mbioni kumhamishia Mbowe jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa polisi hawapaswi kuliita shambulio hilo ni la kawaida kama mengine kwa kuwa kauli hiyo inaziba milango ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

“Viashiria vya tukio vinaonyesha vilikuwa na mlengo wa kisiasa.  Kati ya watu waliomshambulia wapo waliosikika wakimwambia mwenyekiti maneno kwamba ‘tuone kampeni utafanyaje’”, amesema Mnyika.