July 5, 2024

Polisi wasema Mbowe anahojiwa Dar es Salaam kwa makosa ya jinai

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi amesema Mbowe alisafirishwa Jumatano asubuhi kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya makosa ya jinai.

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi amesema Mbowe alisafirishwa Jumatano asubuhi kupelekwa Dar es Salaam.
  • Chadema yaeleza kuwa kukamatwa kwa Mbowe na wafuasi wengine wa chama hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. 

Mwanza. Jeshi la polisi mkoani Mwanza limekiri kumshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe na wafuasi wengine 15 likieleza kuwa kiongozi huyo kwa sasa anashikiliwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kwa ajili ya tuhuma za makosa ya jinai aliyofanya siku za nyuma.

Kauli ya polisi inakuja ikiwa ni siku moja baada ya chama hicho kueleza kuwa kiongozi huyo na wafuasi hao walikamatwa Saa 8:30 usiku akiwa hotelini alikofikia mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi amewaambia wanahabari leo Julai 22 kuwa kiongozi huyo na wengine 15 walipanga kufanya mkusanyiko na uhalifu kinyume cha sheria na kwamba walikamatwa asubuhi na si usiku wa manane. 

Watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa na polisi ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Taifa, John Pambalu, John Heche na aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveri Lwaitama.

Ng’anzi amesema kuwa Mwanza ilipiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima mpaka watu wawe na vibali maalum vya kufanya mikusanyiko hiyo lakini wanachama na viongozi wa Chadema walikuwa “wameandaa kongamano kwa kile walichokiita madai ya kudai katiba mpya”.

“Walizuiwa wasikusanyike bila kibali maalum na hawakutaka kupata kibali hicho halali,” amesema.

Ng’anzi amesema Mbowe alikamatwa na polisi alfajiri na wakati wanaendelea kumhoji alfajiri polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nao walikuwa wanamhitaji kwa makosa mengine.

“Kwa hiyo ile ile alfajiri 1.30 tulimsafirisha kwenda Dar es Salaam ambako ana makosa mengine ya jinai,” amesmea na kuongeza:

“Sasa hivi yupo salama katika kituo cha polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kwa ajili ya makosa yaliyokuwa yakimkabili siku za nyuma.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi akizungumza na wanahabari jijini Mwanza Julai 22, 2021. Picha|Mariam John. 

Kamanda Ng’anzi amesema mwanzoni walipata taarifa kuwa “mkusanyiko ule ungeleta vurugu na uvunjifu wa amani kwa sababu baadhi yao walipanga kufanya vitendo vya kiuhalifu zaidi ya kukusanyika.”

Chadema imelaani kukamatwa kwa kiongozi wao na wafuasi wake kikieleza kuwa hatua hiyo ni ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mapema Jumanne Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel alizuia mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwa ni njia ya kujikinga na wimbi la tatu la ugonjwa wa Uviko-19 ambapo kwa Mwanza ulitajwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Hata hivyo, Chadema kupitia taarifa kwa umma walisema wataendelea na kongamano hilo kwa kufuata taratibu za kiafya zinazoelekezwa na wataalamu.

Kongamano hilo, lililokuwa na ujumbe wa kudai Katiba mpya, lilipangwa kufanyika Julai 21 katika hotel ya Tourist iliyopo maeneo ya kona ya Bwiru wilayani Ilemela lakini jana polisi walitanda eneo hilo na kuzuia lisifanyike.