October 7, 2024

Polisi yawashikilia wanne kwa uhalifu wa kifedha Mwanza

Wanatuhumiwa kuwatapeli wananchi kwa noti za kigeni zisizo halali.

  • Wanatuhumiwa kuwatapeli wananchi kwa noti za kigeni zisizo halali.
  • Wakutwa na Dola za Marekani 192 sawa na Sh441,000.  
  • Kufikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika. 

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kujihusisha na shughuli za utapeli na kubadilisha fedha za kigeni kinyume na sheria mkoani humo. 

Watuhumiwa hao ambao ni Yelemi Athuman (45), Mussa Juma (440), Rutayisile Mande (38) na Deliphina Kungu(51)  wamekamatwa wakiwa na Dola za Marekani 192 sawa na Sh441,000.  

Pia watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na fedha za Kitanzania kiasi cha Sh127,000.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na makaratasi yaliyokatwa mithili ya noti yaliyofungwa pamoja na kuwekwa kwenye bahasha  ambapo waliyatumia kuyachanganya na noti hizo ili kuwahadaa wananchi.

“Watuhumiwa hao walikamatwa jijini Mwanza kwenye mabenki ya kifedha wakiwa na fedha hizo ambapo waliwahadaa wananchi kuwa wanabadilisha fedha kwa kiwango cha chini kulinganisha na kiwango cha ubadilishaji kwa siku hiyo,”amesema Kamanda Muliro

Licha ya kutaja kiwango hicho cha ubadilishaji fedha za kigeni, watuhumiwa hao walikuwa hawatoi kiasi kamili kwa kwa watu kwa sababu walikuwa wanachanganya na makaratasi.

“Mteja anapoona kiwango hicho huzichukua na kumbadilishia anapofika nyumbani ndipo hushtukia mchezo huo,”amesema Muliro.


Soma zaidi: 


Kamanda Muliro amebainisha kuwa watuhumiwa hao siyo tu kwamba wamekamatwa jijini Mwanza isipokuwa mchezo huo wameshaufanya katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Tanga, Kigoma na baadhi ya nchi jirani za Uganda, Zambia na Kenya.

Amesema watuhumiwa hao hutumia mbinu ya kwenda benki  na kujifanya  hawana uelewa na taratibu za kubadilisha fedha ambapo hutaja kiwango cha chini cha ubadilishaji wa fedha kigeni na kuomba msaada kwa mteja waliyemlenga baada ya kubaini kuwa ana fedha nyingi ili awasaidie kujaza fomu.

“Baadaye mteja huyo akikubali na kuingia tamaa ya kupata faida kirahisi wanamrubuni na kutoka naye nje ya benki na kwenda sehemu nyingine ambazo mara nyingi ni maeneo ya hoteli ambapo utapeli huo hufanyika.

“Hujipatia fedha halali za kitanzaia zenye thamani kubwa na wao kumpa anayetapeliwa bahasha yenye makaratasi na wakati mwingine bahasha yenye dola za kimarekani zenye thamani ndogo,” amesema Muliro

Katika tukio la pili, Polisi inawashikilia watu nane kwa tuhuma za kuchana mabango ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo tofauti wilayani Nyamagana.