Prince William atua Tanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wanyamapori
Ni Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza aliyeingia hapa nchini jana atakuwepo kwa siku 4 hadi tarehe 29 Septemba, 2018.
- Ni Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza aliyeingia hapa nchini jana atakuwepo kwa siku 4 hadi tarehe 29 Septemba, 2018.
- Anakusudia kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya ujangiri wa wanayamapori hasa tembo ambao wako hatarini kutoweka.
- Rais Magufuli amuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza.
Dar es Salaam. Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William ameihakikishia Serikali kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha na kuendeleza ushirikiano katika uhifadhi wa wanyamapori na kukabiliana na vitendo vya ujangili dhidi ya tembo ambao wako hatarini kutoweka.
Hayo yamejiri leo, wakati Rais John Magufuli alipokutana na kufanya mazungumzo na Prince William Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Prince William ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, na amemshukuru Rais Magufuli kwa kupata nafasi ya kuzungumza nae.
Prince William amezungumzia juhudi anazozifanya katika uhifadhi wa wanyamapori na amemuomba Rais Magufuli kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ujangili hasa wa tembo.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemkaribisha Prince William kuja nchini wakati wowote na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza ikiwemo kushirikiana nae kuhifadhi wanyamapori.
“Naomba ufikishe salamu zangu kwa Malkia Elizabeth II, mwambie Watanzania tunaipenda Uingereza na tutaendeleza na kuuimarisha zaidi ushirikiano wetu mzuri kwa manufaa yetu sote” amesema Rais Magufuli.
Zinazohusiana:
- Kitulo ‘Bustani ya Mungu’ fahari ya Nyanda za Juu Kusini.
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania.
- Ndani ya Ifisi: Hifadhi ya wanyamapori inayotoa pumziko kwa wakazi wa Mbeya.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na ujangili hasa wa Tembo ambapo kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba anatarajia Prince William ataunga mkono ili kukomesha kabisa ujangili katika hifadhi zote za wanyamapori hapa nchini.
Prince William aliyeingia hapa nchini jana atakuwepo kwa siku 4 hadi tarehe 29 Septemba, 2018.
Kwa mujibu wa ripoti ya Serikali iliyotolewa mwaka 2015, Tembo wa Tanzania wamepungua kutoka 109,051 mwaka 2009 na kufikia 43,330 ilipofika mwaka 2014 ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 60 ya tembo wameuawa.
Hata hivyo, serikali inaendelea na mpango wa kuwafunga vifaa maalum (Elephant tracking system) tembo katika Hifadhi za Taifa kufuatilia mienendo yao ili kukabiliana na tishio la kutoweka kwa tembo hao.
Zoezi hilo limefadhiliwa na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shirika la uhifadhi mazingira duniani (WWF) pamoja na Fredkin Concervation Fund.Kutoka kushoto: Rais John Magufuli akiwa na Prince William ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi. Mwingine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Palamagamba Kabudi. Picha| Ikulu.