October 6, 2024

Programu ya huduma za hali ya hewa yazinduliwa Dar

Programu hiyo inayokusudia kuongeza kasi ya uchakataji, usambazaji na utoaji wa taarifa za hali ya hewa.

  • Programu hiyo inayokusudia kuongeza kasi ya uchakataji, usambazaji na utoaji wa taarifa za hali ya hewa. 
  • Itawafaidisha zaidi wakulima ambao wanategemea mvua kuendeleza shughuli za kilimo. 
  • Pia, itawaleta pamoja wadau wa maendeleo kuangalia namna bora ya kutumia taarifa za hali hewa kwa maendeleo endelevu. 

Dar es Salaam. Wakulima wa Tanzania huenda wakaongeza tija katika uzalishaji wa mazao yao, baada ya programu ya huduma za hali ya hewa inayokusudia kuongeza kasi ya uchakataji, usambazaji na utoaji wa taarifa za hali ya hewa kuzinduliwa Jijini Dar es Salaam. 

Programu hiyo inayojulikana kama “Weather and information Services for Africa” (WISER) imezinduliwa leo (Agosti 29, 2019) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi aliyebainisha kuwa itaanza kutekelezwa Tanzania licha ya kuwa imelenga kutumika Afrika nzima.

Amesema programu hiyo ni muhimu kwa Tanzania kwa sababu inaimarisha juhudi na mikakati iliyopo ya uchakataji na usambazaji wa taarifa sahihi za hali hewa kwa wananchi ili wazitumie katika shughuli za maendeleo hususan kilimo. 

Dk Kijazi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), amebainisha kuwa programu hiyo itajikita zaidi kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za mwenendo wa mvua ili kufanya maamuzi katika shughuli za kilimo.

Programu hiyo ya WISER inakusudia pia kuwajengea uwezo wataalam na kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya utabiri wa hali hewa vitakavyosaidia kuboresha taarifa zinazotolewa na mamlaka za Tanzania ili ziwafaidishe wadau mbalimbali. 

“Programu hii itasaidia kuimarisha shughuli zetu nchini hasa katika sekta mbalimbali na kuisaidia Tanzania kutekeleza adhma yake ya kujenga uchumi wa viwanda,” amesema Dk Kijazi.


Soma zaidi: 


Programu ya WISER, ambayo iliasisiwa mwaka 2015 na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID), inaendesha mikutano na makongamano yanayowakutanisha wadau wa maendeleo na watunga sera kujadili namna nzuri ya kutumia taarifa za hali ya hewa katika shughuli za uzalishaji. 

Mratibu wa WISER kwa nchi za Afrika Mashariki, John Mungai amesema programu hiyo ni muhimu hasa kwa wananchi wa kawaida kwa sababu inatafsiri taarifa za hali ya hewa kwa lugha za wazawa ili waelewe na kuzitumia kwa urahisi katika maeneo yao.

“Licha ya kuwaleta pamoja wadau wa maendeleo, tunataka kuona taarifa za hali ya hewa zinachangia kuleta mabadiliko kwenye jamii,” amesema Mungai wakati akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya WISER leo (Agosti 29, 2019) jijini Dar es Salaam. Picha|Daniel Samson.