October 6, 2024

Raia wa Ubelgiji waombwa kula chipsi mara mbili kwa wiki

Wananchi wa Ubelgiji wameombwa kula chipsi angalau mara mbili kwa wiki kutokana kuwepo zaidi ya tani 750,000 za viazi mviringo ambavyo visipotumika vitatupwa.

  • Hiyo inatokana na kuwepo kwa zaidi ya tani 750,000 za viazi mviringo ambavyo visipotumika vitatupwa.
  • Ulaji wa chipsi umepungua nchini humo kutokana na kufungwa migahawa na baa.

Dar es Salaam.  Wananchi wa Ubelgiji wameombwa kula chipsi angalau mara mbili kwa wiki kutokana kuwepo zaidi ya tani 750,000 za viazi mviringo ambavyo visipotumika vitatupwa. 

Kuwepo kwa ziada ya viazi hivyo kumetokana baa na migahawa mingi kufungwa ili kuwaepusha wananchi na mikusanyiko kipindi hiki ambacho ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ukiendelea kusambaa duniani. 

Pia kwa sasa Serikali ya nchi hiyo inatekeleza marufuku ya watu kutokutoka nje kama tahadhari ya ugonjwa huo hatari. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la CNBC, mamlaka inayosimamia tasnia ya viazi ya Belgapom imesema tani hizo 750,000 za viazi ambazo zinaweza kujaza malori makubwa 30,000 hazitachakatwa kwa sababu ya janga la COVID-19. 

Kutokana na kupungua kwa mahitaji ya viazi, viwanda vya bidhaa hiyo vimepunguza uzalishaji, jambo linalotishia kudhoofika kwa tasnia ya viazi nchini humo. 


Soma zaidi: 


Katibu Mkuu wa Belgapom Romain Cools ameiambia CNBC kuwa ili kuokoa jahazi wanawaomba wananchi kuongeza ulaji wa chipsi angalau mara mbili kwa wiki. 

“Tunachojaribu kufanya ni kuepuka upotevu wa chakula kwa sababu kila kiazi kilichokaangwa ni hasara,” amesema Cools akihojiwa na shirika hilo. 

Ubelgiji ilianza kutekeleza marufuku ya kutokutoka nje nchi nzima Machi 18 mwaka huu ili kupunguza maambukizi ya COVID-19. 

Hadi kufikia jana, nchi hiyo ilikuwa na wagonjwa 46,687 wa Corona huku waliofariki dunia wakifikia  7,207, kwa mujibu wa takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani.