October 6, 2024

Rais Kenyatta akemea ubaguzi Afrika Mashariki

Amesema huwezi zuia wananchi wa Tanzania na Kenya kutembeleana.

  • Rais Kenyatta amesema huwezi zuia wananchi wa  Tanzania na Kenya kutembeleana.
  • Amesema viongozi wanawajibu wa kuondoa vikwazo vyote vya kutembeleana na kufanya biashara.

Dar es SalaamRais wa Jamuhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta amewasili leo chini Tanzania  kwa ziara ya kibinafsi ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine amekemea vikali suala la ubaguzi dhidi ya raia wa nchi hizo mbili.

Katika hotuba yake fupi aliyoitoa baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Chato, Rais Kenyatta amesema wakati wa utawala wake anapenda kuona Afrika Mashariki ikiwa mmoja huku akikimea wanasiasa wanaongea wanaotoa kauli za kibaguzi.

Kauli hiyo ya rais huyo wa Kenya inakuja siku kadhaa baada ya Mbunge wa Starehe jijini Nairobi Charles Kanyi Njagua maarufu kama Jaguar kuwapa Saa 24 wageni wanaofanya biashara katika eneo lake la utawala wakiwemo Watanzania kuondoka mara moja vinginevyo angewafurusha. 

Hatua hiyo ya Jaguar ilipingwa vikali nchini kiasi cha kulifanya Bunge kuitaka Serikali kutolea tamko suala hilo. 

Jaguar tayari alishafikishwa mahakamani nchini humo kwa mashtaka ya uchochezi makosa ambayo ameyakana.

“Wawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kufanya biashara Kenya? Wawezeje mwambia Mtanzania hawezi tembea  Kenya?

“Wawezaje mwambia Mtanzania huwezi tafuta bibi Kenya na vilevile huwezi mzuia Mkenya kuja kufanya biashara yake Tanzania…huwezi kumzuia Mkenya kutembela jirani yake, huwezi mzuia Mkenya akiwa ameona mtoto hapa Chato amnong’oneze kidogo…hiyo ndio Afrika Mashariki tunayotaka sio ile ya kizamani,” amesema Kenyatta huku akishagiliwa na wananchi.

Amesema kama watoto wa Afrika Mashariki, viongozi wanawajibu wa kuondoa vikwazo vyote vya kutembeleana na kufanya biashara huku akieleza kuwa njia  ya kumaliza mipaka na ukabila ni kuona.

Pia amepongeza Rais Magufuli kwa kujenga uwanja wa Chato nakusema uwanja huo utafungua fursa mbali mbali za kibishara.

Kwa upande wake Rais John Magufuli amemsukuru Rais Kenyatta kwa kumtembelea na kusisitiza wao ni ndugu na marafiki.

Dk Magufuli amesema Rais Kenyatta ameweka historia ya kuwa Rais wa kwanza aliye madarakani kwenda katika makao hayo makuu ya Mkoa wa Geita.

“Serikali zetu pia zinashikiana vizuri sana tumekuwa na ushirikiano wa kibalozi toka uhuru…mwaka 2009 tulianzisha tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Kenya,” amesema Rais Magufuli akieleza uhusiano wa muda mrefu na Taifa hilo tajiri zaidi Afrika Mashariki.