November 24, 2024

Rais Magufuli aagiza mashamba ya ngano Manyara yaanze kulimwa

Amesema kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki na kuzuia wawekezaji na wakulima kufaidika na kilimo cha zao.

  • Amesema kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki na kuzuia wawekezaji na wakulima kufaidika na kilimo cha zao.
  • Ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wawekezaji wanaagiza ngano nje ya nchi.  

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza mashamba ya ngano ya mkoa wa Manyara yaendelezwe ili kuwawezesha wawekezaji wanaoagiza zao hilo nje ya nchi wapate malighafi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya uzalishaji katika viwanda vya ndani. 

Rais Magufuli aliyekua akizungumza leo (Agosti 1, 2019) wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kusaga nafaka cha 21 Century Food and Packaging jijini Dar es Salaam, amesema mashamba hayo yamekaa muda mrefu bila kutumika na yanatakiwa yaendelezwe ili kupunguza gharama za kuagiza ngano nje ya nchi. 

“Yale mashamba yasipotee hivi hivi, nitoe wito hata kwa kampuni yako (Mohammed Entrepreses Tanzania Limited-METL) muanze kulima ngano pale, mtakua mmewasaidia Watanzania wengi zaidi wale watakaokuwa mashambani watapata employment lakini it will be very cheap (itakua rahisi sana) kwa sababu kusafirisha ngano kutoka Manyara kuileta hapa na bahati nzuri treni ya kwenda mpaka Moshi ipo,” amesema Rais. 

Ametoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kuwa kiwanda cha 21 Century kinaagiza ngano toka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yake ya uzalishaji. 

Amesema mashamba ya ngano ya Manyara ambayo sasa hayalimwi yaanze kutumika na ikiwezekana kampuni ya METL ipewe ili ilime na kujipatia malighafi kuendeleza viwanda vyake. 

Shamba la Bassotu ni miongoni mwa mashamba saba ya Gawal, Warret, Gidagamowda, Setchet, Mulbadaw na Murjanda yote yakiwa na ukubwa wa ekari 100,000 yako katika Wilaya ya Hanang katika mkoa huo wa Manyara. 

Yalikuwa yanamilikiwa na Shirika la Taifa la Chakula na Kilimo (Nafco) tangu mwaka 1970 lakini yamekuwa yakikodishwa kwa wawekezaji mbalimbali ili kuyaendeleza kwa kilimo cha ngano, lakini matokeo yake yamekuwa hayaridhishi. 


Zinazohusiana: 


Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya METL, Mohammed Dewji amesema kiwanda hicho kinasaga tani 300 za mahindi na tani 1,240 za ngano kwa siku huku kikiwa kimeajiri wafanyakazi 380. 

Kutokana na uhaba wa ngano ndani ya nchi, wawekezaji mbalimbali wakiwemo wa  viwanda vya bia wanalazimika kuagiza ngano nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotegemea malighafi ya zao hilo.