November 24, 2024

Rais Magufuli aingilia kati sakata la makontena ya Makonda

Asisitiza makontena yaliyozuiliwa bandarini lazima yalipiwe kodi kwa mujibu wa sheria.

  • Asisitiza makontena yaliyozuiliwa bandarini lazima yalipiwe kodi kwa mujibu wa sheria.
  • Awataka viongozi kuzingatia sheria kuepuka maslahi binafsi kwenye utumishi wa umma.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli kwa mara ya kwanza amezungumzia sakata la makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yaliyozuiliwa bandarini na kutaka makontena hayo yalipiwe kodi.

Amesema hayo leo Agosti 29 wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo ameagiza sheria za ulipaji kodi lazima zifuatwe na watu wote wakiwemo viongozi wa Serikali.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena ameambiwa alipe kodi, kwanini asilipe?, amesema Rais Magufuli.

Makontena hayo yanayodaiwa kuwa na fenicha za shule zikiwemo meza, viti na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari ya Dar es Salaam na yanatarajiwa kupigwa mnada baada ya kushindwa kulipiwa kodi kutokana na mvutano uliojitokeza kwa wahusika kudai kuwa makontena hayo ni misaada.

Rais amesisitiza kuwa  makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi na kubainisha kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya Serikali na sio Mkuu wa Mkoa.

“Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo,” amebainisha Rais.

Makonda aliingiza nchini makontena hayo yanayokadiliwa kufikia 20 akidai kuwa ni fenicha ambazo zitatolewa kama msaada katika shule mbalimbali zinazokabiliwa na changamoto ya miundombinu. 

Hata hivyo, rais ameweka wazi kuwa viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuepuka mgongano wa maslahi katika jamii. 

“Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine labda wafanyabiashara, unasema ni makontena yako, halafu tena ukasema labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, Maana yake nini?

“Maana yake si unataka utumie walimu, ulete hayo makontena halafu utapeleka shule mbili tatu, ndizo zitapewa mengine unakwenda kuyauza unayapeleka kwenye shopping mall Maduka Makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji masofa, kochi,” amesema.

Kwa mujibu wa TRA makontena hayo yenye umiliki wa Makonda yamekadiliwa kodi ya inayofikia Sh 1.2 bilioni. 

Sakata hilo lilianza baada ya tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, mwaka huu likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 wajitokeze kuzilipia. 

Tangazo hilo lilikuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, ambapo jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DCID yakiwa na samani.