Rais Magufuli akipigia chapuo tena Kiswahili mkutano wa SADC
Amewaomba wakuu wa nchi za Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa hutuba yake kwa Kiswahili ili washawishike kukipitisha kuwa lugha rasmi ya nne ya mawasiliano ya SADC.
- Amewaomba wakuu wa nchi za Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa hutuba yake kwa Kiswahili.
- Amesema hotuba hiyo itawashawishi kuridhia Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC.
- Amesema ni fahari kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaomba Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuridhia na kupitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne itakayokua inatumiwa katika shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo.
Agosti 14, 2019, Lugha ya Kiswahili ilipendekezwa na Baraza la Mawaziri la SADC kuwa lugha rasmi ya nne itakayotumiwa katika shughuli za mawasiliano katika jumuiya hiyo.
Iwapo kitapitishwa na Wakuu wa nchi za SADC katika mkutano unaofanyika leo na kesho, Kiswahili kitaungana na lugha za Kifaransa, Kiengereza na Kireno zinazotumika katika shughuli rasmi za jumuiya hiyo.
Rais Magufuli aliyekua akizungumza leo (Agosti 17, 2019) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa nchi za SADC jijini Dar es Salaam, amesema amewaomba wageni walioshiriki mkutano huo kutoa hutuba yake kwa Kiswahili.
Amesema anaamini hotuba yake ya Kiswahili itawashawishi wakuu wa nchi za SADC kuridhia iwe lugha rasmi ya nne ya mawasiliano katika shughuli za jumuiya hiyo yenye nchi 16.
“Ninawaomba wakuu wa nchi mniruhusu nitoe hutuba yangu ya ufunguzi kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kufanya hivyo mtashawishika kukubali na kukipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC,” amesema Rais Magufuli.
Soma zaidi:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
Amesema Kiswahili kinazungumzwa katika nchi 34 za Afrika na sita za SADC, ambapo imekua lugha inayokua kwa haraka duniani.
Katika hatua nyingine, Rais amesema Tanzania inajisikia fahari kubwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao utaikabidhi nchi hiyo ya Afrika Mashariki uenyekiti ambao utadumu kwa miaka miwili ijayo. Tanzania itakabidhiwa uenyekiti kutoka kwa Namibia.