July 8, 2024

Rais Magufuli amfukuza kazi aliyechana kitabu cha dini Kilosa

Ni mfanyakazi wa idara ya Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Daniel Maleki.

  • Ni mfanyakazi wa idara ya Uchumi ya Halmashauri ya  Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Daniel Maleki. 
  • Rais Magufuli amesema kwa namna yoyote mfanyakazi huyo hawezi kuendelea kuitumikia Serikali tena.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemfukuza kazi rasmi mfanyakazi wa idara ya Uchumi ya Halmashauri ya  Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Daniel Maleki kwa kosa la kuchana kitabu cha dini ya kiislamu hadharani. 

Uamuzi huo ameufanya leo (Februari 11, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa jengo la Manispaa ya Kigamboni na jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni jijini Dar Es Salaam, amesema anafahamu kuwa mfanyakazi huyo alisimamishwa kazi na Waziri wa Tamisemi, Sulemani Jafo lakini yeye anamfukuza. 

“Juzi nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jafo, mtu mmoja kule Kilosa nafikiri alichana kitabu kitakatifu, nashukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi. Lakini mimi namfukuza moja kwa moja, muandikieni barua ya kuondoka moja kwa moja,” amesema Magufuli.


Zinazohusiana:


Raisi Magufuli amesema kwa namna yoyote ile mfanyakazi huyo hawezi kuendelea kuitumikia Serikali kutokana na kitendo alichokifanya cha utovu wa nidhamu. 

“Ashinde kesi,  asishinde huyo siyo mfanyakazi wa Serikali. Hatuwezi tukakaa na wafanyakazi wapumbavu katika Serikali hii. Umechukua jukumu la kumsimamisha kazi lakini mimi namfukuza,” amesisitiza Magufuli. 

Februari 7, 2020, Jafo alimsimamisha Maleki baada ya kuonekana eneo la Uhindini Wilaya ya Kilosa akichana  kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislamu na kuagiza viongozi wa mkoa wa Morogoro kumchukulia hatua zaidi kutokana na kitendo hicho alichokifanya.

Maleki anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.