November 24, 2024

Rais Magufuli amtaka Makonda kurejesha fedha za Tasaf

Asema kama Mkuu wa Mkoa huyo wa Dar es Salaam alichukua fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wakati siyo masikini arudishe hizo fedha.

Rais John Magufuli akiwa na Marais Wastaafu pamoja na Viongozi wengine wa Serikali akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Usalama  katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf uliofanyika leo Februari 17, 2020 katika Kituo cha mikutano cha kimataifa JNICC Jijini Dar es Salaam. Picha| Maelezo.


  • Asema kama alichukua fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wakati siyo masikini arudishe hizo fedha.
  • Asema katika  zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanyika kuanzia Novemba 2015 hadi Juni 2017, Serikali iliweza kubaini uwepo wa kaya hewa 73,651.
  • Makonda ajibu kilichotokea. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka viongozi wa Serikali ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda waliochukua fedha za mpango wa kunusuru kaya masikini za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuzitumia isivyo sahihi kuzirejesha mara moja kwani Serikali haipo tayari kuona fedha hizo zikitumika kinyume na malengo yaliyowekwa.

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) leo (Februari 17, 2020) Jijini Dar es Salaam, amesema katika  zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanyika kuanzia Novemba 2015 hadi Juni 2017, Serikali iliweza kubaini uwepo wa kaya hewa 73,651.

Kati ya kaya hizo, 22, 034 zilithibitika kuwa wana kaya wake siyo masikini, kaya 18,700 ambazo hazikujitokeza mara mbili kupokea ruzuku na kaya 9,903 zilizohamia vijiji/ mtaa/shehia ambapo mpango haujaanza.

Amesema katika zoezi hilo wamebaini baadhi ya viongozi ambao walitumia fedha za Tasaf wakati wao siyo masikini, huku akimtaja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kudai kuwa kama anahusika kuchukua fedha hizo arudishe. 

“Na hapa nafikiri ni miongoni mwa wakina Makonda, ambao walizitumia hizi fedha kwenda safari ya Dodoma wakati siyo maskini na ninaomba kama hilo ndiyo kweli, Makonda azirudishe hizi fedha.

“Kama ni kweli alitumia fedha za Tasaf akaenda nazo huko alikokuwa anaeleza, inawezekana nimemsikia vibaya na yeye hahusiki kwenye kaya maskini, mkae mziangalie hizo fedha lazima azirudishe,” amesisitiza Rais Magufuli katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere (JINCC).

Hata hivyo, Makonda kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika kuwa wakati habari zake zikisambaa kwa kasi juu ya kusika na sakata la Tasaf, Watanzania watumie kasi hiyo hiyo kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi(NEC). 

Aidha,  Rais Magufuli alizitaja Halmashauri 10 zilizoathirika zaidi na kaya hewa ni ikiwemo Songea Manispaa ambayo ilikuwa na wanufaika hewa 2,99, Chamwino (1,840), Kinondoni (1,538), Ilala (1,476), Moshi Manispaa (1,071), Arusha Mjini (851), na Temeke (2,012).

Nyingine ni Dodoma Mjini (1,334), Buhigwe (862) na Morogoro (954) huku akibainisha kuwa hiyo ni aibu kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri hizo.

“Siwatishi, nawahimiza Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Ma-DAS, Makatibu Tarafa, Watendaji Kata kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu wa TASAF kwenye maeneo yenu,itakuwa ni moja ya vipimo vya kujua kwamba unastahili kuendelea na nafasi yako,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: 


Tasaf imetumia Sh1.46 trilioni kutekeleza miradi ya kunusuru kaya masikini katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya mfuko huo kilichoanza kutekelezwa mwaka 2013 na kukamilika Desemba 2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladslaus Mwamanga amesema zaidi ya kaya milioni 1.1 zenye watu milioni 5.2 ziliandikishwa katika mpango huo kupata ruzuku stahiki.

Katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf (2020-2023) Serikali imekusudia kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka asilimia 67 hadi asilimia38, ambapo ruzuku hiyo itatolewa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa watu wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kufikia asilimia 30 ya kaya zilizobaki katika maeneo yote nchini.

Pia amepiga marufuku wanufaika wa Tasaf  kukatwa fedha wanazopewa kuchangia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule na hospitali. 

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali na marais wastaafu; Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi.