Rais Magufuli atangaza siku nne za maombelezo ya waliofariki katika ajali ya Mv Nyerere
Rais amesema katika kipindi hicho cha maombolezo, anaamini kila mtu kwa imani yake atawaombea marehemu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
- Rais amesema katika kipindi hicho cha maombolezo, anaamini kila mtu kwa imani yake atawaombea marehemu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametangaza siku nne za maombolezo kuanzia leo (Septemba 21) hadi 24, 2018 kuwakumbuka waliopoteza maisha katika ajali mbaya ya kivuko cha Mv Nyerere kulichozama katika Ziwa Victoria jana mchana na kuua watu zaidi ya 131 hadi sasa.
Dk Magufuli, aliyekuwa akilihutubia taifa kupitia TBC1 na TBC Taifa, amesema katika kipindi hicho cha maombolezo, anaamini kila mtu kwa imani yake atawaombea marehemu waliopoteza maisha katika ajali hiyo mbaya kutokea katika siku za hivi karibuni.
Rais John Magufuli akihutbia Taifa baada ya kutokea ajali ya Mv Nyerere katika Ziwa Victoria. Video| Ikulu.
Mapema leo Saa 10 jioni, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Lucas Magembe aliiambia Nukta kuwa hadi wakati huo watu 126 walikuwa wameopolewa wakiwa wamafariki huku idadi ya waliohai ikiwa ni 37. Hata hivyo, Kijazi anasema watu 40 wameokolewa wakiwa hai.
Kanali Magembe amesema kuwa uokoaji unaendelea na kwamba baadhi ya majeruhi waliokuwa wamelazwa katika Kituo cha Afya ya Bwisya wameanza kuruhusiwa baada ya kupata nafuu.
Kutokana na ajali hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshawasili kisiwani Ukara kuungana na viongozi wengine wanaosimamia jitihada za uokoaji katika eneo hilo la tukio.
Kituo cha televisheni cha Taifa, TBC1 kimemuonyesha Majaliwa akipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella.
Majaliwa amelazimika kusitisha ziara yake ya siku saba iliyokuwa ikiendelea katika mkoa wa Dodoma, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa leo mchana.