July 8, 2024

Rais Magufuli ateua bosi mpya taasisi ya elimu ya watu wazima

Bosi huyo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Fidelice Mafumiko aliyeteuliwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

  • Ni mtaalamu wa masuala ya elimu Dk Michael  Ngu’mbi aliyekuwa akihudumu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
  • Bosi huyo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Fidelice Mafumiko aliyeteuliwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Dar es Salaam. Taasisi ya Elimu ya Watu  Wazima(TEWW) imempata bosi mpya baada ya Rais John Magufuli kumteua Dk Michael  Ngu’mbi kuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo inayotoa elimu kwa watu wazima na ambao hawakubahatika kupata elimu katika mfumo rasmi wa kielimu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi  wa Mawasiliano ya Rais Ikulu  Gerson Msigwa leo (20 Februari mwaka 2019) inaeleza Dk Ngu’mbi anachakua nafasi ya Dk Fidelice Mafumiko ambaye ameteuliwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Dk Ng’umbi ni mtaalamu wa masuala ya elimu aliyejipatia shahada yake ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza.

Kabla ya uteuzi huo  Dk Ng’umbi alikuwa Mhadhiri Mwandamizi Kitivo cha Elimu Cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Opean Univestity of Tanzania ).

Uteuzi wa Ng’umbi ni mwendelezo wa Rais Magufuli kuteua wasomi kutoka vyuo vikuu nchini katika kuongoza taasisi mbalimbali za umma wakiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo , Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Shukran Manya waliokuwa wakifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rais Magufuli pia amemteua Jaji Stephen Magoiga kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal – FCT). Jaji Magoiga amechukua nafasi ya Jaji Barke Mbaraka Sehel ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. 

Taarifa hiyo ya Ikulu imeleza uteuzi huo wa viongozi umeanza Februaria 19, 2019.