October 6, 2024

Rais Magufuli awaongezea nguvu watendaji kata Tanzania

Awataka kutembea kifua mbele na asiwepo mtu wa kuwanyanyasa kwenye ngazi za utendaji wao.

Rais John Magufuli alikuwa akizungumza leo (Septemba 2, 2019) na watendaji wa kata wa nchini nzima katika viwanja vya Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.


  • Awataka kutembea kifua mbele na asiwepo mtu wa kuwanyanyasa kwenye ngazi za utendaji wao.
  • Wametakiwa kudumisha amani katika maeneo yao na kudhibiti wageni kupata vitambulisho vya utaifa. 
  • Amewataka wawe mabolozi wazuri wa kazi inazofanya Serikali. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli amewataka watendaji wa Serikali za mitaa ngazi ya kata kufanya kazi wakitambua kuwa wao ni wawakilishi wake katika jamii, huku akiwaonya viongozi wanaowanyanyasa na kuwabeza watumishi hao wa umma. 

Rais Magufuli alikuwa akizungumza leo (Septemba 2, 2019) na watendaji wa kata wa nchini nzima katika viwanja vya Ikulu, Jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa kukutana na makundi mbalimbali ya watu katika jamii.  

Amesema watendaji kata ni watu muhimu wanaosimamia shughuli za Serikali katika maeneo mbalimbali nchini na hawapaswi kubezwa wala kudharauliwa. 

“Tunapozungumza mafanikio ya Serikali ninyi ndiyo wasimamizi wa mwanzo katika mafanikio hayo,” amesema Magufuli ikiwa ni mara ya kwanza kwa Rais kukutana na viongozi hao tangu nchi kupata uhuru.

Aidha, Rais Magufuli amewaambia viongozi hao kuwa “Cheo cha Afisa Mtendaji Kata siyo kidogo” na kuwataka kutembea kifua mbele na asiwepo mtu wa kuwanyanyasa katika utendaji wao.

Katika hatua nyingine, Rais amewaonya viongozi wa ngazi za juu wa Serikali wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri kufuata utaratibu pale wanapohitaji kuwahamisha viongozi wa ngazi ya kata.

“Ni lazima pawe na utaratibu maalum. Ni marufuku mtu kufikiria tu ofisini na kumuhamisha mtendaji wa kata, ninyi ni mabosi wa Taifa hili,” amesema.


Zinazohusiana:


Pamoja na hayo, Rais Magufuli amewataka viongozi ngazi ya kata kuhakikisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao unaimarishwa huku akisisitiza juu ya kudhibiti utoaji wa vitambulisho vya utaifa kwa wageni.

“Hakuna shughuli za maendeleo zinazoweza kutekelezwa bila kuwa na amani, ni lazima wananchi wafanye kazi bila bugudha. Nawasisitiza maofisa wanaofanya kazi karibu na mipakani watambueni wageni wanaoingia kwenye maeneo yenu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewahi pia kukutana na viongozi wa dini, wafanyabiashara, wachimba madini na hapo baadaye ana mpango wa kuonana na wafugaji wa Tanzania ili kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli zao. 

Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurian Ndumbago amewaambia watendaji waliohudhuria mkutano huo kuwa wao ni tawi la utendaji na ni askari wa mstari wa mbele katika tawi la utendaji.

Amewaasa kuwataarifu wananchi juu ya shughuli za maendeleo zinazoendelea nchini na  kuwakumbusha wananchi juu ya ulipaji kodi na hata ukusanyaji wa kodi hizo.

“Tanzania ni nchi ya pili katika nchi za afrika katika matumizi mazuri ya fedha za umma. Tuhimize watu kupata risiti, kudai risiti na kutoa risiti.

“Ninyi kama wasemaji kwenye kata, inabidi msimamie haya mambo,” amesema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawawezi kuwa kila mahali.