October 7, 2024

Rais mstaafu Mkapa kuzikwa Julai 29

Atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara baada ya kuaga mwili kwa muda wa siku tatu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam

  • Atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.
  • Zoezi la kuaga mwili litafanyika kwa muda wa siku tatu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
  • Mzee Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa hospitalini. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mwili wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa utaagwa Kitaifa Jumanne Julai 28 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.

Mzee Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali iliyopo jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Majaliwa amesema zoezi la kuaga mwili litafanyika kwa muda wa siku tatu mfululizo ambapo wakazi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na wananchi kutoka maeneo mengine wataanza kuaga kuanzia Julai 26 hadi Julai 28.

“Mwili wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais mstaafu wa awamu ya tatu utaanza kuagwa kuanzia Jumapili Julai 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru ambapo saa 4.00 asubuhi kanisa Katoliki litaongoza ibada na baada ya ibada waombolezaji wataanza kuaga,” Majaliwa amewaambia wanahabari leo Julai 24, 2020 kwenye Makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu amesema Julai 28, 2020 zoezi la kuaga mwili litanyika kuanzia asubuhi hadi saa 6.00 mchana ambapo ataagwa kitaifa. 

     

Saa 8.00 mchana mwili utasafirishwa kwenda Masasi kupitia uwanja wa ndege wa Nachingwea na mazishi yatafanyika kijijini cha Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.


 Zinazohusiana:


Mapema asubuhi Majaliwa alikwenda nyumbani kwa mzee Mkapa Masaki jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa mama Anna Mkapa, mjane wa marehemu pamoja na familia, kwa niaba ya Rais John Magufuli na Serikali.

Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Mkapa atakumbukwa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi wakati wa utawala wake na amekuwa moja ya watu mashughuli katika utatuzi wa migogoro mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki na ukanda wote wa maziwa makuu.