October 6, 2024

Rais Samia aagiza kusitishwa mabavu ukusanyaji mapato Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan amesema mwenendo wa sasa wa kufunga biashara na kufungia akaunti unaua walipa kodi na kuwafanya wahamie nchi za jirani.

  • Asema mwenendo wa sasa wa kufunga biashara na kufungia akaunti unaua walipa kodi na kuwafanya wahamie nchi za jirani.
  • Rais Samia ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuongeza wigo wa kodi, na kutengeneza walipakodi wengi zaidi.
  • Wataalamu wa uchumi wasema utakelezaji wa maagizo hayo “utaponya vidonda”.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kupanua wigo wa makusanyo ya kodi na kutengeneza walipa kodi wengi zaidi badala ya kutumia mabavu katika ukusanyaji fedha hizo ikiwemo kufungia akaunti jambo linalowakimbiza wafanyabiashara. 

Katika hotuba yake baada ya kuwaapisha mawaziri wapya wanane, manaibu mawaziri wanane na Katibu Mkuu Kiongozi Hussein Katanga leo Rais Alhamisi (Aprili1, 2021) Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia amesema mwenendo wa sasa wa ukusanyaji mapato unaua biashara na kuwafanya wengine kuhamia nchi jirani. 

Kauli hiyo ya Rais imekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko lukuki kutoka wafanyabiashara juu ya uwepo wa baadhi ya maofisa wa kodi wanaotumia mabavu katika kukusanya mapato ikiwemo kuwafungia biashara. 

Awali Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimuagiza Dk Nchemba kufanya kazi kwa bidii ili kufikia wastani wa (makusanyo ya kodi ya) Sh2 trilioni kwa mwezi kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Mnaua wafanyabiashara”

“Waziri wa Fedha umepewa kigezo hapa cha Sh2 trilioni kwa mwezi, muende mkatanue wigo wa kodi lakini mtengeneze walipakodi wengi zaidi. ‘Trend’ (mwenendo) mnayokwenda nayo sasa hivi ni kuua walipa kodi, mnaua wafanyabiashara, mnatumia nguvu zaidi kuliko akili na maarifa kupata kodi,” amesema Rais Samia. 

“Sasa wale mnaowakamua mkaenda kuchukua vifaa vyao vya kazi, mkafungia akaunti zao, mtachukua fedha kwa nguvu katika akaunti kisa sheria inakuruhusu ufanye hivyo, akitoka hapo anakwenda kufunga biashara anahamia nchi ya pili, mnapunguza walipa kodi,” amesema Rais Samia.

Mara baada ya maagizo hayo, wafanyabaiashara wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa iwapo maagizo hayo yatatekelezwa kikamilifu yatawaletea ahueni katika biashara zao huku wakionya kuwa bidii inahitajika zaidi kupanua wigo wa kikodi kwa kuwa kuongeza walipakodi si jambo rahisi.


Wafanyabiashara watoa ya moyoni

Mfanyabiashara kutoka Kariakoo Peter Mashauri ameiambia Nukta kuwa endapo maagizo hayo yatafuatwa, wafanyabiashara watafanya kazi kwa amani kama ilivyokuwa zamani kwa kuwa kwa sasa hali sio nzuri kwao na inakatisha tamaa.

Mashauri amesema awali waliohusika kukusanya na kufanya ukaguzi wa mapato walikuwa maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) pekee ambao ilikuwa ni rahisi kukuelewa hata pale kosa linapokuwa limefanyika. 

Hata hivyo, kwa sasa Mashauri amesema polisi wanazunguka Kariakoo wakitafuta watu wa kuwakamata huku hata trafiki wakiwa na uwezo wa kusimamisha magari barabarani kwa ajili ya kukagua risiti.

“Ukinunua kitu, kukisafirisha hadi ufike unaokoenda utakaguliwa mpaka uchoke…wakati mwingine wanakuja kama wateja wanajifanya wananunua kitu ilimradi tu wakukamate. Mitaji imeshapotea na kuirudisha siyo kazi rahisi,” ameelezea Mashauri.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimuapisha Balozi Hussein Othman Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo. Picha| Ikulu Mawasiliano.

“Siyo rahisi kihivyo”

Mfanyabiashara mwingine kutoka Kariakoo ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe amesema hii si mara ya kwanza kwa ahadi hiyo kutolewa na kiongozi wa juu kwa kuwa ilishawahi kutolewa awali na Hayati Rais John Magufuli na mambo ndio yalizidi kuwa mabaya.

“Siyo rahisi kama unavyofikiria. Haya mambo siyo mara ya kwanza yanaagizwa lakini bado watu wanafungiwa biashara na akaunti zao zinafungwa,” amesema mfanyabaishara huyo kuwa kuna kipindi Hayati Magufuli alipokutana na wafanyabiashara aliagiza pia maofisa kodi kutotumia mabavu kukusanya mapato.


Soma zaidi:


Wachumi wasema itaponya vidonda

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa maagizo hayo ni ahueni kwa wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla kwa kuwa yataponya vidonda vya wafanyabiashara waliiothirika na mifumo ya kukusanya mapato iliyokuwa ikitumika awali ikiwemo kufungwa kwa akaunti za wafanyabiashara na makato kuchukuliwa kwa lazima katika akaunti za wafanyabiashara hao.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Raphael Maganga ameiambia Nukta kuwa awali wafanyabiashara walipitia madhira ambayo yalisababisha kufungwa kwa biashara zao na kukata kabisa ari ya biashara. 

Maganga amesema wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kwa namna Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikikusanya makato yao.

“Walikuwa wakilalamika wanafungiwa biashara, wanafungiwa akaunti na hiyo imesababisha biashara nyingi kufungwa,” amesema Maganga kwa njia ya simu ambaye ni Msaidizi Mkuu wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Ameeleza kuwa TPSF imekuwa ikishauriana na Serikali juu ya malalamiko ya wafanyabiashara hivyo agizo la Rais Samia linatoa matumaini mapya kwa wafanyabiashara na sekta binafsi.