November 24, 2024

Rais Samia aahidi kutatua changamoto za mahakama Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba mahakama ya Tanzania zikiwemo za uchakavu wa miundombinu.

  • Amesema anatambua muhimili huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu.
  • Amesema Serikali itazipatia ufumbuzi kadiri inavyopata fedha.
  • Awataka majaji kutenda haki katika shughuli zao. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba mahakama ya Tanzania zikiwemo za uchakavu wa miundombinu huku akiwataka majaji kuwa mstari wa mbele kutoa haki kwa Watanzania. 

“Nataka niwaahidi kwa kadri Serikali itakavyokuwa inaongeza uwezo, tutajitahidi kuziondoa changamoto zinazowakabili tukijua kwamba Mahakama ni mhimili wenye dhima ya kutenda haki na kuleta ustawi wa jamii ya Watanzania,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo Mei17, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha majaji 23 wakiwemo Majaji wa Mahakama za Rufani nane na wa Mahakamu Kuu 15 ambao wanaenda kuongeza nguvu kazi katika mhimili huo.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema anatambua kuwa bado mahakama ina changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa mahakimu, uhaba na uchakavu wa miundombinu, vitendea kazi, maslahi ya majaji na mahakimu na mambo mengine madogo madogo. 

Aidha, amesema haki ndiyo msingi wa maendeleo kwenye Taifa lolote hivyo amewasihi  majaji walioteuliwa wakatekeleze majukumu waliyopewa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kuzingatia kiapo walichoapa leo. 

“Nawaombeni mkaongoze vyema lakini mkaongozwe vyema na nafsi zenu. Katika utendaji wa haki, kanuni na sheria zetu zinazotungwa na Bunge na kuja kwenu ni asilimia 70 ya kazi yenu lakini asilimia 30 mkaongozwe na utu na imani zenu na imani zenu,” amesema Rais Samia.


Soma zaidi:


Mama Samia amewaambia majaji hao endapo nafsi zao zikiwatuma kuchukua fedha na kudhurumu haki ya mwingine na kumpa mwingine, wajue watakuwa wameshatetereka na endapo watagundulika, watakua wamekosa sifa ambazo zimewapandisha walipofikia.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema ongezeko la majaji hao litapunguza kiasi cha mashauri ambacho yalikuwa yakisikilizwa na kila jaji na hivyo kuongeza kasi ya kusikiliza mashauri tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Mzigo wa kazi wa kila jopo utapungua kutoka mashauri 956 katika majopo matano yaliyokuwepo hadi 685 kwa majopo saba ambayo tunayo sasa,” 

Pia amesema majaji saba wa Mahakama ya Rufani waliochaguliwa kwa sasa, watapunguza mzigo wa kila jaji wa rufaa na mrundikano wa mashauri.

Zaidi, Prof Juma amesema kuongezeka kwa mashuri katika mahakama ni kwa sababu wananchi wanafahamu haki zao na hivyo matumizi ya mahakama yameongezeka.