July 8, 2024

Rais Samia alivyowafundisha vijana Tanzania kupambania mambo yao

Ahoji ni wapi vijana hukutana na kujadili masuala yanayowahusu?

  • Ahoji ni wapi vijana hukutana na kujadili masuala yanayowahusu?

Mwanza. Wengi walifika asubuhi na mapema katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Hapa kazi ilikuwa moja tu, vijana kuzungumza na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Tofauti na mikutano mingine ya ziara ya Rais Samia jijini hapa, washiriki wa mkutano huu kwa kiwango kikubwa walikuwa ni vijana waliotoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya kanda ya ziwa.

Vijana wengi nchini walikuwa wakisubiria kwa hamu mkutano huo wa vijana na kiongozi huyo wa juu wa nchi ikizingatiwa kuwa ndilo kundi ambalo alikuwa hajazungumza nalo tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.

Walitazamia kuwa wawakilishi wa vijana hao ‘wangetema nyongo” ipasavyo kwa kubainisha na kuchambua matatizo lukuki yakiwemo ukosefu wa ajira, uhaba wa mitaji ya biashara, kodi na tozo lukuki katika  uanzishaji biashara na uwezeshaji wa kisera katika masuala ya kijamii na uwekezaji.

Wawakilishi waliopanda jukwani hapo walimuomba Rais Samia kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa wenye elimu na wasio na elimu ili kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.

Kikwazo kingine ambacho vijana hao walisema ni ugumu wa kulipa mikopo ya elimu ya juu hususan kwa familia maskini na kuwataka vijana wenzao kudumisha amani.

Hata baada ya vijana kuwasilisha hoja zao, baadhi ya vijana hawakufarahia namna masuala yao yalivyowasilishwa kwa Rais Samia.

“Vijana walipewa nafasi kuongea kwa niaba yetu ila hakuna hata mmoja aliyeongea ajenda inayowakabili vijana mpaka pale mama akaongea ajenda mwenyewe,” Dickson Kamala, mmoja wa wanaharakati wa masuala ya vijana nchini Tanznaia aliandika kwenye ukarasa wake Twitter baada ya mkutano huo.

“Kiufupi Mama kaongea na vijana,” aliongeza.



Rais Samia ‘aupiga mwingi’ kuliko vijana

Katika mkutano huo, Rais Samia ndiye alionekana kujadili kwa kina matatizo yanayohusu vijana baada ya kuyainisha vema na kutaka vijana kubadilika.

Kwa lugha za vijana wa sasa, Rais Samia jana “aliupiga mwingi” kuliko vijana wenyewe.  

Rais Samia alisema yupo serikalini kwa muda mrefu hajawahi kuona vijana wakikaa pamoja kwenye jumuiya zao kupembua hoja na mijadala mbalimbali ya kitaifa ikifanyika wakichambua faida na hasara zake.

Kubwa linalofanyika kwenye jumuiya hizo, kwa mujibu wa Rais Samia ni kusherekea chaguzi, kuwabeba wagombea lakini yale yanayowagusa hawayafanyi na kuwaonya kuacha mara moja.

Amesema yapo majukwaa mengi ya kisiasa ambayo yanatumika kuelezea changamoto zao lakini kwa vijana suala hili limesahaulika.

 “Mahali hapa tumekutana wengi ni vijana, ni wapi mnakutana kama vijana, kujadili mambo yenu na kuweka ajenda za kitaifa? Kwa mktadha huu mnanikumbusha kuangalia namna ya kuunda baraza la vijana,” alisema Rais Samia.

Nani anapeleka mambo yenu jumuiya za kimataifa? 

Kiongozi huyo, aliyekuwa akihitimisha ziara yake ya siku ya tatu, pia aliwataka vijana kutoa mwelekeo chanya kwenye ushiriki wa mambo mbalimbali ya kimataifa na kupata mrejesho wake.

 “Mshawahi kufikiri ni nani anayepeleka mambo yenu kwenye mikutano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Madola na UN, nani anayekwenda? Ninachokijua kuna taasisi zisizo za kiserikali ndio zinazokwenda ingawa mrejesho hawajui wanapeleka kwa nani,”amesema Samia.

Baadhi ya vijana waliohudhuria mkutano wa mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza. Picha|Mariam John/Nukta. 

Katika kutatua matatizo mengi ya vijana, Rais ameagiza kuundwa kwa baraza la vijana litakaloshughulikia masuala yanayowahusu vijana zikiwemo ajenda mbalimbali za kitaifa.

Alisema anatambua kuwepo kwa ajenda zao zenye mlengo wa kisiasa lakini kwenye baraza hilo anataka kuona kwanza ajenda za kitaifa.

Boresheni sera ya vijana

Mbali na baraza, Rais Samia alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Sera, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu kuhakikisha wanaboresha sera ya vijana ambayo ilitungwa toka mwaka 2007.

Amesema kupitia maboresho hayo vijana wataweza kutoa maoni yao ikiwemo matumizi ya mitandao, afya na mengine ambayo wakati inatungwa hayakuwepo.

Katika hatua nyingine aliwataka vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili iwanufaishe na si kufanya marumbano na shutuma ambazo zisizokuwa na ushahidi.

Benki ya wajasiriamali mbioni

Kuhusu upatikanaji wa mitaji ya biashara kwa vijana, Rais Samia alisema alizungumza na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dk Akinwumi Adesina aliyeahidi kuongeza vyuo vya veta na kuanzisha benki ya wajasiriamali nchini ili kutatua changamoto ya mitaji.

Vijana waliokuwepo uwanjani hapo wameiambia Nukta Habari kuwa hotuba ya rais na maagizo yake yamewagusa zaidi vijana kuliko walivyotarajia.

Vijana wayakubali ‘madini’ ya Rais Samia

 “Ni kweli ni miaka mingi na karne zimepita vijana hatuna jukwaa la kuzungumzia changamoto zetu na kutoa maoni yetu, Rais katukumbusha jambo la msingi hivyo tunapaswa kuchangamka ili kuunda umoja wenye nguvu,” amesema Abel Rutabyoya mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza.

Anamery Samson amempongeza Rais Samia kwa kutoa mwelekeo wa kupatikana kwa mtaji wa uhakika ambao anaeleza utaenda kuwa mkombozi kwa vijana na kuweza kumudu changamoto zinazowakabili.

Amesema vijana wengi bado wapo vyuoni na hata waliomaliza vyuo miaka minne iliyopita wanasota mtaani hivyo mitaji itawatoa kwenye mkwamo wa ajira na kujiajiri.

Nyongeza na Nuzulack Dausen (Dar es Salaam).