Rais Samia kuunda kamati ya wataalamu kuhusu Corona Tanzania
Amesema anakusudia kuunda kamati ya wataalamu wachunguze kwa undani suala la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) ili iishauri Serikali hatua madhubuti za kuchukua.
- Kamati ya wataalamu itachunguza kwa undani suala la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
- Itatoa mapendekezo kwa Serikali namna ya kulishughulikia suala hilo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema anakusudia kuunda kamati ya wataalamu wachunguze kwa undani suala la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) ili iishauri Serikali hatua madhubuti za kuchukua.
Rais Samia ameeleza leo Aprili 6, 2021 baada ya kuwaapishwa makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za umma na kusema Tanzania siyo kisiwa.
“Kuhusu suala la Covid nakusudia niunde kamati ya wataalamu waliangalie suala la Covid-19 kwa upana wake. Waangalie remedies (suluhu) wanazosema zitatusaidia kwa upana wake kitaalamu kabisa halafu watushauri Serikali,”
“Halifai kulinyamazia. Aidha kulikataa au kulikubali bila kufanya utafiti kitaalamu. Tutafanya tafiti za kitaalamu. Tutaunda kamati ya kitaalamu. Watuambie upeo wa swali au tatizo hili lilivyo na hayo yanayopendekezwa na ulimwengu kuja kwetu,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
- Hakuna kulala: Rais Samia afanya mabadiliko makubwa vigogo taasisi za Serikali
Kamati hiyo, kwa mujibu wa Rais, itasaidia kubaini ukweli wa jambo hilo kwa kutumia wataalamu wa ndani.
“Hatuwezi kujitenga kama kisiwa na hatuwezi tu kupokea yanayoletwa kwetu bila kufanya utafiti wa kwetu. Rais (Jakaya) Kikwetea aliwahi kutuambia “Akili za kuambiwa? Changanya na zako” kwa hiyo tuweke na zetu tuwe na msimamo maalum unaoeleweka. Siyo tunasoma mambo ya Covid ulimwenguni, Tanznaia desh, desh, haieleweki. Tueleweke kama tunakubali, tunakataa. Tunafanyaje. Tueleweke,” amesema kiongozi huyo wa juu zaidi nchini.
Kauli hiyo ya Rais Samia ni ya kwanza kutolewa kuhusu masuala ya Covid-19 tangu alipoingia madarakani Machi 19 kufuatia kifo cha Hayati Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.