November 24, 2024

Rais Samia Suluhu aeleza alivyomfahamu hayati Magufuli

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema anamfahamu binafsi hayati Rais John Magufuli kama kiongozi mchapakazi, mfuatiliaji, mnyenyekevu, mwalimu na aliyekuwa na maono makubwa ya kuboresha maisha ya Watanzania.

  • Anasema alikuwa mchapakazi, muadilifu, mfuatiliaji na aliyeweka maslahi ya Taifa mbele.
  • Pia alikuwa mtu mcheshi na mwenye utani, jambo lililowavutia wengi kufanya naye kazi.
  • Viongozi mbalimbali wamesema Tanzania imempoteza kiongozi muhimu aliyekuwa na maono ya kulifikisha mbali Taifa lake. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema anamfahamu binafsi hayati Rais John Magufuli kama kiongozi mchapakazi, mfuatiliaji, mnyenyekevu, mwalimu na aliyekuwa na maono makubwa ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Rais Samia ameeleza kuwa amezifahamu sifa hizo nzuri na nyingine za Dk Magufuli tangu alipoanza kufanya naye kazi akiwa Waziri. 

“Nilipata fursa ya kumjua Rais Magufuli nilipopata fursa ya kuhudumu kama Waziri wa Muungano ndani ya Muungano wa Jamhuri wa Tanzania. Nilihusudu uchapa kazi wake namna alivyokua mfuatiliaji mzuri wa wizara yake ya ujenzi na hata alipokuwa uvuvi. Alibeba jukumu hili kwa uzito ulio sahihi,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi.  

Rais Samia ametoa ushuhuda huo leo Machi 22, 2021 jijini Dodoma wakati wa kumuaga kitaifa hayati Magufuli, shughuli iliyohudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.

Katika hotuba yake iliyopangiliwa vizuri, Rais Samia amesema, Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo, alisimama kama Mtanzania halisi aliyeweka maslahi ya Taifa mbele kuliko binafsi na familia yake. 

Kutokana na dhamira hiyo ya kulitumikia Taifa lake, Dk Magufuli alifanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi mkubwa kuhakikisha Watanzania wanahudumiwa vizuri.

“Nilivutiwa na namna alivyotoa michango yake Bungeni na kwenye Baraza la Mawaziri, Niliona dhamira yake kama mtu anayependa kazi yake. Alijua barabara zote za nchi hii kwa majina, urefu na fedha zilizotumika kuzijenga,” amesema.


Soma zaidi:


Rais Magufuli hakuogopa kutetea kile alichokiamini kilicho sahihi kwa maslahi ya Taifa hata kama kingehatarisha maslahi yake. 

Mama Samia, ambaye aliapishwa Machi 19 mwaka huu, amesema Rais Magufuli alimpa fursa ya kuonyesha uwezo wake na kuwa wanawake wanaweza ikiwa watajengewa mazingira ya kufanya kazi kisawa sawa.

“Inanipa faraja katika miaka sita alinipa nafasi kuhudumu kama msaidizi wake wa kwanza na wa karibu,” amesema Rais Samia aliyekuwa makamu wa Rais wa Tanzania tangu mwaka 2015, Magufuli alipoingia madarakani. 

Alikuwa mcheshi na mwenye utani

Sifa nyingine aliyokuwa nayo hayati Magufuli alikuwa mcheshi na mwenye utani, jambo liliwafanya watu wengi kuwa karibu yake ili kujifunza uchapa kazi wake. 

“Kwa wengi alijulikana kama “a nonsense person” (mtu asiyependa masihara) ila kwa upande mwingine Mheshimiwa Magufuli alikuwa mcheshi na mwenye utani sana. 

“Mara nyingi kazi zikimpungukia anatupigia simu na akipigia anauliza mume wako, mkeo yupo hapo nipe niongee naye. Na alikuwa ana utani sana, hilo nalo lilitusogeza karibu na yeye na tukaweza kufanya kazi kwa karibu zaidi,” amekiri Rais Samia ambaye anakuwa Rais mwanamke wa kwanza Tanzania. 

Mama Samia, ambaye alikuwa akiongea kwa unyenyekevu huku wananchi waliofurika katika uwanja wa Jamhuri wakimsikiliza kwa makini, amesema Magufuli alikuwa mchapa kazi aliyefanya kazi usiku na mchana huku “bidii yake ilikuwa mithili ya mchwa.”

Gari lililobeba mwili wa Hayati Magufuli ukiingia katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Picha| Msemaji Mkuu wa Serikali.

Alipenda matokeo kuliko visingizio

Kutokana na haiba yake ya uchapa kazi, hayati Magufuli alipenda kuona matokeo yenye tija kutoka kwa watu aliowangoza hasa katika kuwatumikia Watanzania wanyonge. 

“Alipenda kuona matokeo na matokeo ndilo jibu pekee alilopenda kusikia kwetu na siyo visingizio na lawama. Alitukumbusha kuwa maisha yake ni sadaka kwa Watanzania, hivyo hakuwa na budi kufanya kazi usiku na mchana kuwaletea Watanzania maendeleo,” amesisitiza Rais Samia na kubainisha kuwa;

“Sote tuliohofia sana iwapo alipata muda wa kupumzika au kuwa na familia. Alifanya haya yote kutokana na bidii yake, uzalendo na upendo wake kwa Watanzania na nchi yake.”

Tabia hizo zikawa chachu kwa viongozi walio chini yake kuendana na falsafa yake ya “Hapa Kazi Tu” ambayo inahamasisha utendaji kazi wa viwango na tija kwa wananchi. 

“Tumepoteza kiongozi mahiri, shupavu, jasiri, mchapa kazi, muadilifu, mnyenyekevu, mcha Mungu, mfuatiliaji, mzalendo, mtetezi wa wanyonge, mwana wa Afrika, mwanamapinduzi wa kweli,” amesema Mama Samia ambaye alikuwa akishangiliwa mara kwa mara kila alipomtaja hayati Magufuli katika hutuba yake.

Aidha, amesema wataendeleza mazuri yote aliyoacha Rais Magufuli ambaye kesho ataagwa visiwani Zanzibar na kisha kupelekwa jijini Mwanza kabla ya kuzikwa Chato mkoani Geita Machi 26, 2021.