November 24, 2024

RC Chalamila atangaza maombi maalum kumuombea Rais Magufuli

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza katika ibada maalum ya kumuombea Hayati Rais John Magufuli itakayofanyika katika uwanja wa Sokoine kesho Machi 19, 2021.

  • Amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza katika ibada maalum ya kumuombea Hayati Magufuli itakayofanyika katika uwanja wa  Sokoine kesho Machi 19, 2021.
  • Amesema maombi hayo pia yatakuwa ni ya kuliombea Taifa, Mwenyezi Mungu aendelee kulilinda na kuliweka mikononi mwake. 

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza katika ibada maalum ya kumuombea Hayati Rais John Magufuli itakayofanyika katika uwanja wa  Sokoine kesho Machi 19, 2021. 

Rais John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu kwa maradhi ya moyo.

“Siku ya kesho Machi 19, 2021 Serikali ya Mkoa wa Mbeya imeandaa ibada maalum itakayofanyika uwanja wa Sokoine ambayo ibada hii itajumuisha viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali, itajumuisha wananchi, machifu, viongozi mbalimbali waandamizi wa mashirika ya umma na yasiyo ya umma na vyama vya siasa.

“Lengo ni kuwa na maombi maalum katika uwanja huo wa Sokoine kumuombea Rais wa Tanzania kupata pumziko la milele na pumziko lenye heri,” amesema Chalamila mbele ya wanahabari leo Machi 18, 2021 jijini Mbeya.

Amesema maombi hayo pia yatakuwa ni ya kuliombea Taifa, Mwenyezi Mungu aendelee kulilinda na kuliweka mikononi mwake ili Watanzania na hasa wana Mbeya wasivurugane katika kipindi chote ambacho Taifa liko kwenye majonzi makubwa.  


Soma zaidi:


Aidha, amewataka wananchi wa mkoa huo kupokea kifo cha Magufuli aliyefarikiwa akiwa na umri wa miaka 61 kwa mikono miwili na kwa sababu  Mwenyezi Mungu ndiye aliyeyaruhusu yatokee.  

“Tuendelea kuwa wastahimilivu katika kipindi chote cha maombolezo na kuendelea kumuombea sana Rais wa Tanzania yaani Dk John Magufuli,” amesisitiza mkuu wa mkoa huyo. 

Pia amewataka kumuombea Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwa na nguvu ya kubeba msiba huu hadi pale mazishi yatakapofanyika na mpaka hapo tena taratibu nyingine za kisheria zitakapoendelea.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Mama Samia ndiye atakua Rais kwa kipindi kilichobaki ambaye atachagua makamu wa Rais atakayefanya naye kazi mpaka mwaka 2025. 

Chalamila alikuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali waliojitokeza siku chache zilizopita kukanusha uvumi kuhusu afya na alipo Rais Magufuli, pale watumiaji wa mitandao ya kijamii walipokuwa wanaishinikiza Serikali kuwapatia majibu kwa kile walichodai kuwa hajaonekana hadharani na wana haki ya kujua yuko wapi.

Machi 12, Chalamila alisema alimpigia simu Rais Magufuli, na kumshukuru kwa ajili ya miradi kadhaa aliyoipokea mkoani kwake na aliwataka watu wenye nia ovu kuacha kumzushia Rais kuwa anaumwa kwani Rais ni mzima na anaendelea kutekeleza miradi ya Tanzania.