November 24, 2024

RC Mwanza apiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Roberth Gabriel amepiga marufuku mikusanyiko ya vikundi mkoani Mwanza visivyokuwa na ulazima ili kujikinga na ugonjwa wa Corona (Uviko-19) wimbi la tatu.

  • Amesema hiyo itasaidia kupunguza maambukizi ya Uviko-19.
  • Aagiza watu kuvaa barakoa, kunawa mikono.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Roberth Gabriel  amepiga marufuku mikusanyiko ya vikundi mkoani Mwanza visivyokuwa na ulazima ili kujikinga na ugonjwa wa Corona (Uviko-19) wimbi la tatu.

Gabriel aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Julai 20, 2021, amesema katika kuendelea kujikinga na ugonjwa huo kuna mambo ya kufanyia marekebisho ikiwa ni pamoja na utoaji elimu pamoja na suala la ufuatiliaji.

Katika suala hili la ufuatiliaji, kiongozi huyo amesema hakuna ulazima wa kuwepo kwa mikusanyiko isiyo ya lazima na katika maeneo yanayowakutanisha watu kama kanisani, misikitini au sokoni watu wahakikishe wanavaa barakoa.

“Niwaombe viongozi wa wilaya, tarafa na kata kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji kwenye maeneo hayo, mtu anapoenda sokoni hakikisha kuna ndoo za kunawia mikono na amevaa barakoa  ili wakati wanapobadilishana fedha isiwepo namna inayoweza kusababisha maambuki,” amesema Gabriel

Ameagiza viongozi wa wilaya kuzingatia utoaji wa vibali vya kufanya mikusanyiko kwenye maeneo yao huku akiweka ulazima uvaaji barakoa maeneo mbalimbali kama misibani, sokoni na kwenye ofisi za  serikali kabla ya kumhudumia mtu.

“Mwanza ni mkoa hatuwezi kucheza na maisha ya watu ni lazima tuzingatie maelekezo na kutoa elimu ya watu kujikinga na kupeana nafasi,” amesema.

Pia ameagiza kuwepo kwa vifaa vya kunawia mikono na vitakasa mikono kwenye maeneo ya shule na kama hakuna wahakikishe wanaweka huku wananchi wakitakiwa kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari.

Anasema wakiendelea na kampeni hii ndani ya miezi mitatu ijayo hali inaweza kuwa tofauti kwa kuwa Mkoa wa Mwanza unatajwa kuathirika na janga hili kuliko mikoa yote Tanzania.

Amewataka wasafiri wasiogope kufika na kuwa wachukue tahadhari, na kwamba matamasha, mikutano ya hadhara  ya kisiasa na mingine itakuja baadaye.