July 8, 2024

REA yawakalia kooni wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini

Wakala wa Umeme Vijijini (REA) umesema utavunja mikataba kama kazi walizopewa hazitakamilika kwa wakati.

  • Yasema itavunja mikataba kama kazi walizopewa hazitakamilika kwa wakati. 
  • Pia imevunja mkataba na mkandarasi kutoka kampuni ya Nipo Group.
  • Mkandarasi huyo ameshindwa kupeleka umeme katika vijiji 139.

Mwanza. Huenda wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini wataongeza umakini na kuzingatia mikataba yao, baada ya Serikali kuongeza kibano kwa wakandarasi wanaochelewesha kazi walizokabidhiwa. 

Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imevunja mkataba na mkandarasi kutoka kampuni ya Nipo Group  baada ya kushindwa kutekeleza kwa wakati mradi wa awamu ya tatu ya usambazaji wa umeme vijijini katika Mkoa wa  Mwanza. 

Kampuni hiyo ilipewa tenda ya kusambaza nishati ya umeme katika vijiji 139 vilivyopo katika Mkoa wa Mwanza kwa kuhakikisha inakamilisha uwekaji wa miundombinu ikiwemo nguzo na kutandaza nyanya kwenye maeneo yatakayopitiwa na mradi huo.

Lakini haijakamilisha kazi hiyo kama ilivyokubaliwa katika mkataba. 

Uamzi wa kusitisha mkataba huo umefikiwa kwenye kikao cha pamoja kilichoikutanisha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuazimia  kuvunja mkataba huo na kuagiza kazi aliyokuwa anaitekeleza mkandarasi huyo kwa bàadhi ya vijiji aendelee kuikamilisha.

Katika awamu ya tatu zaidi ya Sh1.56 trioni  zilitengwa kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji vilivyokuwa vimelengwa katika mikoa 25 nchini Tanzania ikiwemo ya Arusha na Kigoma ambapo ukomo wake ulikuwa Juni mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Mwanza, Mwenyekiti wa  Bodi hiyo, Kalolo Bundala  amesema  Mkandarasi huyo ametekeleza wastani wa asilimia 40 tu ya mradi aliokabidhiwa. 

“Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na Mkandarasi huyo kutotimiza wajibu wake kikamilifu, hivyo tunaamua kuvunja mkataba huo na sasa mradi huo utatekelezwa na kampuni tanzu ya  Shirika la Umeme Tanesco la ETDCO,” amesema Bundala. 


Soma zaidi: 


Kabla ya kuchukua uamuzi huo, amesema menejimeti ilikaa na kuona upo umuhimu wa kumpunguzia kazi mkandarasi huyo ambapo pia hata yeye alishirikishwa suala hilo na kuridhia na kuwa yote ni kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati.

Mpaka sasa kampuni hiyo haijavifikia vijiji 79 na vijiji 69 ambavyo ilivifikia, kazi haijakamilika. 

Meneja wa ETDCO, Mhandisi Madea Mbonile amesema atahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ifikapo Septemba mwaka huu ili kutoa nafasi kwa mradi mwingine kutekelezeka kwa mzunguko wa tatu.

Mkurugenzi Mkuu REA, Amos Maganga amesema zoezi hilo ni endelevu kwa wakandarasi katika mikoa mingine ambao wamekabidhiwa kazi ya kusambaza umeme vijijini na hawajakamilisha kwa wakati.

Amesema mikataba yao itavunjwa na watapewa watu wengine wenye uwezo wa kuitekeleza kwa wakati.