October 7, 2024

Redio za umemejua zinavyoinua elimu Kenya

Zinawasaidia wanafunzi kupata elimu wakati huu ambao shule zimefungwa kutokana na janga la Corona.

  • Wanafunzi wanapata masomo kwa kusikiliza vipindi vya redio zinazotumia nishati ya umemejua.
  • Zinasaidia kukabiliana na athari za COVID-19 kwenye sekta ya elimu.

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Kenya, limegawa redio 10,000 zinazotumia nishati ya umemejua kwa kaya masikini nchini humo ili watoto wengi wapate fursa ya kusoma nyumbani wakati huu wakijiandaa kurejea shuleni Januari mwakani.

Wanaofaidika na kifaa hicho ni pamoja na Selina Nakesa Mamati anayeishi katika eneo la mtaa wa mabanda la Kibera jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa Radio ya Umoja wa Mataifa (UN), Selina ni mwanafunzi  wa sekondari ambaye hakwenda shuleni kwa miezi 8 iliyopita na yuko nyuma kimasomo.

Lakini sasa mambo yatabadilika kwani Selina ni miongoni mwa watoto 40,000 wanaofaidika na msaada huo wa redio za umemejua (sola) baada ya UNICEF kutambua athari za kufungwa shule wakati huu wa COVID-19 hasa kwa kaya masikini. 

Mkuu wa mawasiliano wa shirika hilo nchini Kenya, Andrew Brown ameiambia redio ya UN kuwa, “kufungwa kwa shule kumeingilia masomo kwa mamilioni ya wanafunzi nchini Kenya ambao wamekosa zaidi ya miezi sita ya masomo rasmi na wakati huo wote tumeisaidia Serikali kwanza kwa watoto kusomea nyumbani na pili kwa maandalizi ya shule kufunguliwa kwa usalama.” 


Zinazohusiana:


Redio hizo ambazo ni rahisi kutumia zinawawezesha watoto kusikiliza masomo redioni na kuwawezesha kuelimika hata wakiwa nyumbani. 

“Redio hii ya sola imemisaidia sana kwa sababu kuna vitabu ambavyo nasoma shuleni vinaitwa Kigogo, tunapokuwa shuleni tunavisoma, lakini kupitia Redio wanavisoma na pia wanatuelezea kwa kina hivyo naweza kuunda picha halisi katika fikra zangu ili niweze kuelewa vyema,” amesema Selina. 

Ingawa ni shule chache zilizofunguliwa nchini humo, UNICEF imesema inaendelea kusaidia wanaosomea nyumbani hadi pale shule zote zitakapofunguliwa kwa usalama. 

Umemejua ni miongoni mwa nishati endelevu na safi ambazo jumuiya ya kimataifa imekua ikipigia chapuo kutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia na kupata mwanga ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.