Sababu nne za kutofautiana kwa matumizi ya umeme majumbani
Sababu hizo ni pamoja na tabia zisizofaa za watumiaji wa umeme, makundi ya watumiaji na aina ya vifaa vya kielektroniki vinavyotumika ndani ya nyumba.
- Baadhi ya tabia zinazoathiri mwenendo wa matumizi ya umeme katika nyumba ni pamoja na kuwasha vifaa vya kielektroniki kama friji, feni, viyoyozi, pasi au televisheni bila ulazima wa kufanya hivyo.
- Kutokugua mfumo wa umeme wa nyumba kwa muda mrefu husababisha umeme kupotea na kushindwa kufika eneo husika kirahisi.
- Utofauti wa makundi ya wateja na aina ya vifaa vya umeme kinachotumika huathiri mwenendo wa umeme ndani ya nyumba.
Dar es Salaam. Umeunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa katika nyumba yako? Lakini bado una maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu matumizi sahihi ya viwango vya umeme ukilinganisha na jirani yako ambaye umeme wake unakaa muda mrefu licha ya kuwa na matumizi yanayofanana, jambo ambalo linakufanya utumie gharama kubwa kununua umeme kila mara ili kukidhi mahitaji ya nyumba yako.
Hali hiyo inachangiwa na sababu mbalimbali za kibinadamu na kitaalamu ambazo zikiepukwa zinaweza kusaidia kuokoa gharama za kununua umeme wa ziada ambazo zingetumika katika shughuli zingine. Hizi ndio sababu nne za kutofautiana kwa matumizi ya umeme majumbani:
Tabia za kibinadamu zisizofaa za matumizi ya umeme
Zipo tabia mbalimbali ambazo zinachangia matumizi ya umeme kutofautiana kutoka nyumba moja hadi nyingine. Tabia hizo ni pamoja na kuwasha vifaa vya kielektroniki kama friji, feni, viyoyozi, pasi au televisheni bila kuvitumia.
Hapa ninazungumzia tabia ya baadhi ya watu kuacha radio au televisheni ikiwaka siku nzima na hakuna mtu anayesikiliza wala kuangalia. Haya ni matumizi mabaya ya nishati ya umeme katika nyumba yako, washa vifaa vya kielektroniki pale inapohitajika.
Tabia nyingine ni kuziacha taa zikiwaka kwa muda mrefu hata katika nyakati za mchana ambapo jua linatoa mwanga. Lakini wapo ambao wanawasha na kuzima friji na taa mara kwa mara. Fahamu wazi kuwa umeme unatumika zaidi wakati kifaa kinawashwa, kwahiyo kila unapozima na kuwasha unazidisha kiwango cha umeme kinachotumika.
“Hakikisha unapotumia pasi usiiache ikiwaka ukaenda kufanya kazi nyingine. Vyivyo hivyo tutumiapo hita za kuchemshia maji na majiko ya umeme,” unaeleza mwongo wa usalama wa shirika la umeme (Tanesco).
Matumizi sahihi ya taa yanaweza kusaidia kuokoa umeme unaopotea katika nyumba. Picha| Business Insider.
Lakini tabia nyingine hatarishi kwa matumizi ya umeme ni kuweka vitu vingi kwenye friji kuzidi uwezo wake. Hii husababisha friji kutumia umeme mwingi kupita kawaida ili kupooza vitu ulivyohifadhi. Unashauriwa kuweka vitu kwa wastani ili kulipa uhai zaidi friji lidumu muda mrefu ujao.
Kwa wanaotumia majiko ya kupikia ya umeme nao wanapaswa kufahamu kuwa ikiwa sufuria ni kubwa kuliko sahani (plate) ya jiko, umeme utakaotumika utakuwa mwingi zaidi ya sufria la kawaida linaloendana sahani ya jiko.
Mabadiliko ya tabia ni muhimu ili kuokoa umeme unaopotea kwa matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaweza kuepukwa na fedha zinazotumika kununua umeme wa ziada zitumike kwa shughuli zingine za maendeleo.
Zinazohusiana:
- Megawati 300 za umeme wa upepo kuchagiza uchumi wa viwanda.
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya taifa.
- Namna umeme unavyoweza kuchochea maendeleo vijijini.
Ukaguzi wa mifumo ya umeme ndani ya nyumba
Mifumo ya umeme katika nyumba isipokaguliwa na kufanyiwa matengeneza kwa muda mrefu inasababisha kukatika au kulegea kwa nyaya na viunganishi kama soketi, swichi. Hali hii husababisha umeme kupotea na matokeo yake mtu hulazimika kununua umeme mwingi kuliko matumizi halisi ya nyumba yake.
Pia fyuzi ya umeme ikikatika au soketi breka ikajizima, hahakikisha unamwita fundi kukagua kwa nini ilizima ili kubaini tatizo lililojitokeza.
Tanesco wanashauri kuwa, “Tuhakikishe tunamwita mkandarasi aliyesajiliwa kupitia mfumo wote wa umeme kwenye nyumba (hasa maungio yote) kila baada ya miaka mitano. Tusiongeze vitu vinavyotumia umeme mwingi kama viyoyozi bila kuwahusisha makandarasi waliosajiliwa kuangalia uwezo wa mifumo yetu ya umeme kuhimili mzingo unaoongezeka.”
Fyuzi ya umeme ikikatika au soketi breka ikajizima, hahakikisha unamwita fundi kukagua kwa nini ilizima ili kubaini tatizo lililojitokeza. Picha| Arrive Alive.
Makundi ya watumiaji
Kwa mujibu wa Tanesco, bei ya umeme inatofautiana kutokana na kundi la matumizi ya mteja alilopo. Wateja wa matumizi madogo ya nyumbani wanaotumia umeme wa majumbani ambao matumizi yao ni wastani wa kilowati 75 kwa mwezi wananunua umeme uniti moja kwa Tsh100 (bila kodi) endapo watazidi hapo kila unit watatozwa Sh350 bila kodi.
Kwa wateja wa kundi la matumizi ya kawaida ambao hujumuisha wateja wenye matumizi ya kawaida ya umeme hususani watumiaji majumbani, biashara na viwanda vidogo, taa za barabarani na mabango wananunua umeme uniti moja Sh292 (bila kodi) ambapo kundi hili linatumia umeme kuanzia uniti 75 hadi 7500 kwa mwezi.
Kutokana na utofauti huo wa makundi ya matumizi husababisha matumizi ya umeme kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine licha ya kutoa kiasi cha pesa kinacholingana.
Aina ya vifaa vya umeme vinavyotumika kwenye nyumba
Kadiri nyumba inavyokuwa na vifaa vingi vya kielektroniki ndivyo matumizi ya umeme yanazidi kuwa makubwa. Lakini vifaa hivyo hutofautiana kilowati za umeme zinazotumika. Ndio maana unashauriwa kuangalia kwa makini nguvu ya umeme ya kifaa unachonunua ili kuhakikisha matumizi yake yanaendana na bajeti yako.
Matumizi ya taa ambazo zinajulikana kama “Energy saver” yanashauliwa kutumika katika nyumba kwasababu zinatumika kiasi kidogo cha umeme.