November 24, 2024

Sababu za Ali Mafuruki kujiuzulu uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Vodacom

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, Ali Mafuruki ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Desemba 1, 2019 ili apate muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.

  • Ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Desemba 1, 2019 ili apate muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.
  • Alijiunga na Vodocam Tanzania Agosti 1, 2017.
  • Vodacom yasema ametoa mchango mkubwa kwa kampuni hiyo. 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, Ali Mafuruki ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Desemba 1, 2019 ili apate muda zaidi wa kuendelea na biashara zake. 

Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo Oktoba 18, 2019, imeeleza kuwa Mafuruki ameitumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili na baada ya mwezi mmoja ujao ataachia nafasi hiyo ya uenyekiti. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mafuruki ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Infotech Investment Group ameamua kuchukua uamuzi huo ili apate muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.  

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa kampuni hiyo, Caroline Mduma ameeleza kuwa Mafuruki alijiunga na Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania Agosti 1, 2017 na katika kipindi chote alichofanya kazi na bodi hiyo ametoa mchango mkubwa kwa kampuni na uongozi kwa ujumla.

“Bodi inatumia nafasi kumshukuru kwa mchango na uongozi wake mahiri na tunamtakia kila heri katika shughuli zake,” amesema Mduma katika taarifa hiyo. 


Zinazohusiana:


Mafuruki aliwahi kuwa pia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mwananchi Communications Limited, Benki ya Stanbic na Mwenyekiti wa  taasisi ya Africa Leadership Initiative East Africa Foundation.