July 5, 2024

Sababu za kwa nini unatakiwa kusamehe maishani

Usiposamehe unabaki kwenye kifungo cha chuki huku kinyongo chako kikikutafuna wewe mwenyewe.

  • Kusamehe kutakupatia amani ya moyo.
  • Endapo hautosamehe, ni wazi kuwa utajenga chuki na mtu.
  • Unaweza kujifunza kusamehe kwa wepesi kwa kusikiliza sababu za makosa kufanyika.

Ni kosa gani ambalo ukifanyiwa na mtu hautomsamehe hata mwezi ushuke duniani? Kama lipo, ni vyema kuanza kufikiria kama upo ulazima wa wewe kuishi maisha yako na kinyongo dhidi ya mtu mmoja.

Ni kweli kama wanadamu duniani, tumeumbwa na tofauti zetu ambazo zinatufanya kuwa watu wa kipekee yani Mike awe Mike na Jane abaki kuwa Jane. Tofauti hizo zinaweza kuwa ni za kitabia, kimawazo na namna ya kuchanganua mambo ambapo huo ndio ubinadamu wenyewe. 

Miongoni mwa watu, wapo ambao ni wepesi kusamehe pale wanapokosewa hata iwe ni kosa kubwa kiasi gani. Lakini pia, wapo ambao kosa moja ambalo mtu atalifanya dhidi yake, litafuta mema yote ambayo mtu ameyatenda kwake katika kipindi ambacho wamefahamiana.

Kama wewe kusamehe ni jambo jepesi kwako, hongera sana, kwa ambaye kusamehe ni mtihani wa maisha, ni matumaini yangu andiko hili litabadilisha msimamo wako.

Kusamehe kunakuacha ukiwa na amani na kukupunguzia makasiriko. Picha| The Daily Beast. 

Kwanini usamehe? Kwa maoni yangu, hizi ndio sababu za wewe kukatilia mbali kinyongo chako.

Kusamehe kutakupatia amani ya moyo

Hii imeongelewa sehemu nyingi  vikiwemo vitabu vya dini. Imani zote zinatufundisha kuwa chuki, kisasi na kutokusamehe sio jambo linalohakikisha mwisho mwema kwetu.

Mfano, endapo haujamsamehe mtu, huwa unapata hisia gani pale unapokutana naye? Bila shaka utatumia dakika mbili tatu kukumbuka mambo aliyoyafanya na kutamani atoweke mbele ya macho yako. Chuki yako juu yake itakua siku hadi siku na utajikuta unatenda dhambi bila kujua.

Endapo utajifunza kumsamehe na kuendelea na maisha, bila shaka uwepo wake hautokuumiza moyo wala kukutendesha dhambi zisizo na msingi.

Unapoombwa msamaha kuwa mwepesi kusamehe kwani hata wewe utahitaji kusamehewa. Picha| Inspirationalfeed.

Utajifunza kutokana na makosa

Pengine kutokusamehe kwako kunakuacha ukining’inia kwenye chuki badala ya kuangalia kitu cha muhimu zaidi ambacho ni mafunzo ya makosa uliyotendewa.

Mara kadha abinadamu tunajiweka katika nafasi ya kulaumu pale baya linapofanyika juu yetu na kusahau umuhimu wa kutafuta sababu ya ubaya husika.

Kuna wakati mwingine inaweza kuwa ni matendo yetu ndio yamehamasisha ubaya hivyo kuna haja ya wewe kujirekebisha pia. Samehe, tafuta chanzo cha kosa na kitatue.

Utaboresha mahusiano

Endapo kila kosa likifanywa kwako unabaki na kinyongo na mtu huyo maishani mwako, utashikilia mangapi?

Mkurugenzi wa Utafiti na Elimu katika Chama cha Glendon nchini Marekani, Dk Lisa Firestone, PhD kupitia tovuti ya masuala ya kisaikolojia, ya psychalive ameandika kuwa msamaha ni kitovu cha mahusiano.

Katika andiko lake Dk Firestone amesema msamaha ni ufunguo wa kujenga mahusiano yenye afya hivyo unapojifunza kumsamehe aliyekukosea, unakuwa unayaboresa mahusiano hayo.

Wahenga walisema “wagombanao ndio wapatanao”. Ni dhahiri mapatano yanapofanyika, mahusiano huwa thabiti zaidi na unakuwa umejifunza kitu kutoka kwa aliyekukosea. 

Unaweza kuchukulia hali ya kutokuelewana kama chumvi kwenye mahusiano na kama njia ya kumuelewa mtu zaidi. Hivyo unapokosewa, jitahidi kufikiria mema kuliko mabaya.

Unaposamehe, unaimarisha mahusiano. Picha| Lifelong Learner.

Mbinu za kukusaidia kusamehe kwa urahisi

Hapa inategemea na kosa ambalo umefanyiwa lakini ni vyema kujua kuwa, kama binadamu, hatujakamilika na kukosea ni sehemu ya ubinadamu. Kabla haujaamua kumfuta mtu katika maisha yako, tambua kuwa, na wewe wapo uliowakosea na huenda hata hawakukuambia.

Gazeti la kuchapisha habari za mitindo maisha la “Greater Good” limeorodhesha njia nane za kusamehe kwa urahisi. Kati ya njia hizo ni pamoja na kufahamu msamaha ni nini na una umuhimu gani.

Kwangu mimi msamaha ni kuganga yajayo na kujifunza na ya kale lakini pia ni njia yangu ya kuendelea kushika uskani wa maisha yangu.

Kuna wimbo wa Shawn Mendes na Justin Bieber, “Monster” ambapo mstari wa Bieber unasema “unforgiveness keeps them in control” ambayo tafsiri yake ni “kutokusamehe kunawapa guvu dhidi yako”. Kwangu, kipande hicho kimeshikilia wimbo wote.

Unaposamehe inamaanisha kumuona mtu aliyekukosea haitokuumiza wala kukufedhehesha hivyo unakuwa na nguvu ya maamuzi. 

Kwa upande mwingine, usiposamehe, uliyemkosea amekushinda.

Greater Good limeandika, unaweza kusamehe kwa wepesi kwa kutafuta ushauri wa watu wenye hekima ambao pia hawana chuki lakini muhimu zaidi kujifunza kutokana na makosa.

Vijana wa siku hizi wanasema “YOLO” ikimaanisha “You Only Live Once” ambayo tafsiri yake ni kuwa unaishi mara moja tu hivyo badala ya kuyafanya maisha hayo kuwa ya kinyongo na watu, ni vyema ukajifunza kusamehe watu ili kutokuwa na majuto katika siku zako za kuishi zilizobaki.

Kwa leo, tuishie hapa. Tukutane wiki ijayo hapa hapa www.nukta.co.tz