November 24, 2024

Sababu za Serikali ya Tanzania kusitisha bei mpya za vifurushi

TCRA yasema usitishaji huo utatoa nafasi kwa watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kina kwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji.

  • TCRA yasema usitishaji huo utatoa nafasi kwa watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kina kwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji.

Dar es Salaam. Angalau sasa watumiaji wa huduma za intaneti Tanzania watapata ahueni kutokana na Serikali kusitisha matumizi ya bei mpya za vifurushi vya data ili kuvipita upya kulinda maslahi ya watumiaji ikiwa ni ndani ya Saa 24 baada ya kampuni za huduma za simu kubadili vifurushi hivyo.

Tangu mapema asubuhi ya Aprili 2, 2021 ambayo ni siku rasmi ya kuanza kwa tozo hizo mpya za vifurushi, watumiaji wa huduma za simu nchini wamelalamikia kupunguzwa kwa kiwango kikubwa cha vifurushi ikiwa ni kinyume na matarajio yao.

Wadau mbalimbali walianzisha kampeni ya kupinga mabadiliko hayo wakitumia viunganishi mbalimbali (Hashtags) ikiwemo #InternetMustFallTZ.


Inayohusiana: 


Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusitisha kutumika kwa gharama hizo mpya hasa katika vifurushi vya data ili kuweza kuvipitia upya na kuleta huduma rafiki.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba ameeleza katika taarifa yake ya jioni ya Aprili 2 mwaka huu kuwa watoa huduma waliwasilisha idadi na bei ya vifurushi vipya pamoja na bei za huduma nje ya vifurushi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni mpya ndogo na kuidhinishwa na mamlaka hiyo.

“Hata hivyo, TCRA imesitisha kwa muda matumizi ya bei mpya ya vifurushi vya data ili kutoa nafasi kwa watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kina kwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji,” amesema katika taarifa hiyo kwa umma.

Kusitishwa kwa bei hizo mpya za vifurushi vya data kunafanya uamuzi huo kuwa moja ya maamuzi ya haraka kufanywa na uongozi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Machi 19 kufuatia kifo cha Hayati John Magufuli.