July 3, 2024

Sababu za Tanzania kufufua zao la michikichi

Serikali imesema imeamua kulipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini ili kukidhi mahitaji ya ndani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Dk Filson Kagimbo kuhusu uoteshaji wa mbegu bora za michikichi wakati alipotembelea kitalu cha miche ya michikichi cha kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichpo wilayani Kigoma, Februari 21, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asema litsaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.
  • Awataka vijana kuchangamkia fursa za kuzalisha zao hilo.
  • Aitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kuzalisha na kusambaza mbegu bora za michikichiki. 

Dar es Salaam. Serikali imesema imeamua kulipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, hivyo ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ziada itakayobakia itauzwa nje ya nchi.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi hasa vijana kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa upo uhakika wa kupata mbegu bora na pia zao hilo litawakwamua kiuchumi na kuwaondolea umasikini wa kipato.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo (Februari 22, 2020), uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo katika kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kihinga mkoani Kigoma unaendelea vizuri na unaridhisha. 

Upatikanaji wa mbegu bora utawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji katika maeneo yao ili kujipatia soko la uhakika la zao hilo ambalo linahitajika kwa wingi nchini ili kuzalisha mafuta ya kula yanayoagizwa nje ya nchi.

“Amewaagiza Maofisa Ugani kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwaelekeza namna ya kulima zao hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji mashamba, matumizi bora ya pembejeo ili waweze kulima kisasa na kujiongezea tija,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ikimnukuu Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Februari 21, 2020) alipotembelea kituo cha Tari cha Kihinga mkoani Kigoma.


Soma zaidi:


Akiwa kituoni hapo, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utafiti juu ya uendelezaji wa zao la michikichi uliofanywa na Tari kuanzia mwaka 2018 hadi Februari 15, 2020, unaonyesha kuwa taasisi hiyo imezalisha mbegu milioni 1.52 ambazo zinaweza kupandwa katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30,500.

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zenye mazingira mazuri ya uzalishaji wa michikichiki lakini inakadiriwa kuwa inaagiza tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese na hutumia takriban Sh600 bilioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia pengo la uhaba wa mafuta.

Licha ya changamoto za uzalishaji wa zao hilo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na soko, uzalishaji wa mawese umekuwa ukiongezeka kila mwaka jambo linalotoa matumaini kwa Serikali na wadau wa zao hilo kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji.

Hali ya hewa ya Tanzania inaruhusu michikichi kustawi kwa wingi hasa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya (Wilaya ya Kyela) na Pwani ambayo ina hali ya kitropiki hasa joto la wastani na mvua za kutosha.