Sababu za vijana kukimbilia mafanikio ya haraka Tanzania
Ni pamoja na presha ya mitandao ya kijamii na wazazi na kuanza majukumu wakiwa katika umri mdogo.
- Ni pamoja na presha ya mitandao ya kijamii na wazazi.
- Kuanza majukumu wakiwa katika umri mdogo.
- Pia kushindwa kuwa na malengo ya muda mrefu.
Dar es Salaam. Hakuna kijana ambaye hafikirii kupata mafanikio katika maisha yake. Kama yupo, basi huenda ni mmoja kati ya 100 na anastahili kuzawadiwa kisiwa akaishi peke yake. Natania!
Katika umri wa kuanzia miaka 20, vijana huwaza kumiliki gari, biashara ya kuingiza kipato au ajira ambayo inamlipa mshahara mkubwa ili aweze kujenga nyumba yake na kuwasaidia wazazi wake.
Kiu hiyo ya kuona kuwa maisha yanaenda mseleleko inawafanya vijana wengi kutokuukubali uvumilivu na uhalisia wa kwamba hata uhuru wa Tanganyika haukupatikana kwa jitihada za siku moja bali ulipatikana kwa mchakato wa muda mrefu na huenda ni zaidi ya ule historia inaoueleza.
Siku za hivi karibuni, nilipata muda wa kusikiliza simulizi ya ndugu yangu kuhusiana na safari yake ya kufikia mafanikio.
Yeye alianza kwa kuuza miwa kijijini na alikuwa akitembea umbali mrefu sana kufika mjini ambapo alikuwa na uhakika wa wateja. Kadiri siku zilivyoenda, aliona kuwa miwa haina mzunguko mkubwa kwani muwa mmoja alikuwa akiuuza Sh10 hadi Sh50.
Licha ya kuwa angeweza kuondoka na Sh100 kwa siku, bado mzunguko wake ulihitaji nguvu ya ziada ikiwemo kupiga kelele za kuita wateja na kutembea hapa na pale. Kipindi hicho alikuwa na miaka 18.
“Nilikuwa na hamu sana ya kufanya biashara. Mimi sikusoma lakini niliamini lazima nitafanikiwa tu na hakuna yeyote wa kunisaidia bali jitihada zangu,” ni maneno ya baba yangu mdogo wakati akinipa wosia wa maisha.
Kufikia kuwa na duka Kariakoo na kumiliki mali pamoja na kusomesha ndugu wengi, ilikuwa ni mchakato mrefu wa kuyatafuta mafanikio hatua kwa hatua bila kupita njia ya mkato.
“Ninaujua uchungu wa pesa kwa sababu nimeitafuta kwa jasho na ni jasho kweli,” ameniambia hayo wakati akinielimisha juu ya matumizi mazuri ya pesa na nguvu ya uvumilivu katika maisha akinionya kutokutumia pesa kwenye anasa.
Ujana ni maji ya moto na hutaka kuzifikia ndoto zao haraka lakini uhalisia wa maisha huwapunguzia spidi ya kufika katika ndoto zao. Picha|Unsplash.
Kwa nini mafanikio ya haraka?
Kuna sababu nyingi ambazo zinawachochea vijana hasa walio chini ya miaka 30 kuyatafuta mafanikio kwa nguvu na wakati mwingine kutaka “shortcut” kuyapata na hivyo kujihusisha na biashara zisizofaa au kushawishika kufanya yasiyostahili ambayo ni mada ya siku nyingine.
Baadhi ya sababu ni kama ifuatavyo:
Majukumu katika umri mdogo
Kwa baadhi ya vijana, majukumu na utegemezi kwa siku hizi huanza wakiwa na umri mdogo hasa kwa ambao wamebahatika kuingia vyuoni.
Matarajio ya wazazi wengi, unapokuwa mjini na baada ya kumaliza chuo ni kuwa utapata ajira na utasaidia wanaokufuata wakiwemo wadogo zako na ndugu na hata wazazi kama wana kipato kidogo.
Lipate hili kwa usahihi. Hakuna anayependa kuombwa fedha na mzazi wake iwe ya hospitalini, matumizi binafsi na kadhalika kisha amjibu kuwa hana pesa. Hiyo ni kawaida miongoni mwa vijana wengi wa Kitanzania.
Jambo hilo huwafanya vijana kufanya kila linalowezekana kupiga madili ya hapa na pale na hata kupoteza dira ya kutimiza ndoto zao kwa kutimiza haja za muda mfupi na kusaidia wale wanaowatizamia.
Soma zaidi:
- Haya ndiyo makosa yanayowamaliza vijana wengi wakati wa kuomba kazi
- Sababu za vijana kutochangamkia fursa za kujiunga na vyama wa wafanyakazi
- Fursa zinazoweza kuwapa ahueni vijana wasio na ajira Tanzania
Presha kutoka kwa rafiki na mitandao ya kijamii
Unaweza usikubaliane na hili lakini hata wewe kutoka moyoni, fikiria ni mara ngapi umepata hamasa ya kufanya kitu kwa sababu fulani anafanya au umejiuliza fulani amewezaje kufanikiwa akiwa na umri huo na wewe bado?
Binafsi ninawaona rafiki zangu wakipiga hatua kubwa kubwa na kutoka moyoni, ninanajiuliza “eh aisee mimi nipo nyuma sana” wengine tayari wanafamilia huku wengine wakishikilia nyadhifa mbalimbali za juu huku wakiendelea kunifikirisha na post zao za mitandaoni.
Leo ana gari hili, kesho yupo hoteli hii na kadhalika. Mafanikio yao hayaniumizi bali yananifikirisha kujua wapi mimi ninakwama kufikia ndoto zangu. Hili huenda lipo kwa baadhi ya vijana.
Kwa wengi, jambo hili linaweza kuwafanya wapoteze dira na waanze kufanya hata kazi ambazo hawazifurahii ilimradi tu wanalipwa vizuri.
Na hapo ndiyo mwanzo wa kuona utu uzima kuwa mgumu na mchachu kama ndimu mbichi.
Kuficha uhalisia wao
Hakuna asiyetamani kuyapatia maisha. Ni wachache sana watakubaliana na hali yao mbele ya rafiki, ndugu na jamii yao kwani licha ya shida zote ambazo mtu anaweza kuwa nazo, baadhi yao huendelea kutabasamu.
Hili siyo geni nadhani. Katika jamii zetu kuna misemo kama “fake it untill you make it” ambayo tafsiri yake kwa Kiswahili ni “igiza hadi yatimie” kwa baadhi, msemo huo ndiyo husababisha mtu kuonyesha kuishi maisha mazuri ambayo hawezi kuyamudu ili tu kufurahisha wanaomzunguka.
Asichokijua mtu huyo ni kuwa, wakati ananufaisha umma, yeye anajiumiza na kuwa watu hawatakumbuka jitihada zake za kuwaridhisha pale siku akianguka bali watakumbuka madhaifu tu.
Zipo sababu zingine nyingi zikiwemo tamaa, mahusiano, hurka binafsi, na mengine mengi ambayo nikiyaandika yote, huenda tukatumia siku nzima kuyasoma.
Usininukuu vibaya, kufatuta mafanikio siyo jambo baya, swali linakuja, “Mafanikio hayo unayatafuta vipi?”
Kwa leo, ninakupa muda wa kutafakari hayo ili kama umeangukia katika kundi moja wapo, upate muda wa kuwa nami wiki ijayo siku kama hii ambapo nitakuletea maoni kutoka kwa viongozi wa dini, wazazi na hata wanasaikolojia kuhusu suala hilo.
Endapo una swali unataka lijibiwe, wasiliana nami kupitia mitandao ya kijamii @NuktaTanzania kwa Twitter, Instagram na hata Facebook.